top of page

Kumfuata Kristo Katika Dunia Isiyojali Ukristo: Kubeba Msalaba Wetu Kila Siku

Updated: Jul 1

Mwongozo wa Kujifunza Maisha, Kifo, na Ufufuo wa Yesu Kristo

Kunguru wawili wameketi juu ya msalaba dhidi ya anga nyeupe. Picha ya rangi nyeusi na nyeupe, ikitoa hisia ya utulivu na taharuki.

🏹Wito wa Ufuasi Usio na Mipaka


Yesu alisema kwa uwazi, "Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, abebe msalaba wake kila siku, na anifuate." (Luka 9:23). Huu si mwaliko wa mara moja kwa wiki au wa siku ya ibaada tu. Ni mwito wa maisha kamili—kutembea kila siku katika upendo wa kujitoa, upendo wa aina ya msalaba. Si kanisani tu, bali nyumbani, sokoni, kwenye mitandao ya kijamii, hata vijiweni mtaani.


Tunaishi katika kizazi ambapo Injili haitambuliki tena kama dira ya maadili ya jamii, bali imepunguzwa kuwa sauti ya pembeni isiyosikilizwa. Kwa mujibu wa N. T. Wright katika Surprised by Hope, tunaishi kati ya Pasaka na Ufunuo: kati ya ufufuo wa Kristo na uumbaji mpya unaokuja. Katika dunia hii ya baada ya Ukristo, ambapo makanisa hayaonekani tena kama sauti kuu ya jamii, ufuasi wa Yesu unahitajika kuonekana katika maisha ya kila siku ya huduma, ushuhuda na ujasiri.

Swali kuu: Tutamfuata Yesu kwa uaminifu vipi, bila kupotea katika vishawishi vya dunia ya sasa inayomsahau Kristo?

Makala haya ni kama darubini—kutusaidia kuona njia ya kweli ya kumfuata Yesu katika dunia yenye kelele na vishawishi.



🌍 Kuishi Ufalme wa Mungu Katikati ya Giza la Kitamaduni


Ingawa dunia ya wakati wa mitume haikujua maandiko kwa mapana, kanisa la kwanza liliwaka kwa nguvu ya kiroho iliyozidi elimu ya kawaida. Wakiwa hawana vyuo wala seminari, walihubiri kwa maisha yao, huduma zao, na maombi yao ya kila siku. Tofauti na wao, sisi tunaishi katika jamii ambazo zilishawahi kupuliziwa na harufu ya Kikristo lakini sasa zinazikwepa harufu hiyo kana kwamba ni mzigo. Zamani, hata sheria za kijiji ziliakisi mafundisho ya Biblia. Leo hii, burudani imechukua nafasi ya sala, na mitandao ya kijamii imeziba sauti ya waamini. Imani ya Kikristo inaonekana kama vizuizi vya uhuru badala ya lango la uzima wa kweli.

  • Katika elimu: Maadili ya Kikristo yameondolewa kwenye mitaala au yanapingwa kama yasiyo jumuishi.

  • Katika burudani: Maudhui ya kidini yanatupwa pembeni, huku dhihaka dhidi ya imani zikipewa nafasi.

  • Katika mitandao ya kijamii: Ushuhuda wa imani hukabiliwa na kejeli, mashambulizi au kupuuzwa.

  • Katika siasa: Maamuzi ya msingi wa kiroho huonekana kama vitisho dhidi ya “uhuru binafsi.”

  • Katika jamii: Wakristo wanaotangaza msimamo wa imani huchukuliwa kuwa wa nyuma au wasio na huruma.

Wakristo wengi wanaogopa kujitofautisha. Wengine wanaenda na mkondo wa dunia hadi hawatofautiani tena na wale wasiomjua Yesu. Hatari ni hii: Tusije tukajichanganya kiasi cha kupoteza utambulisho wetu kama wafuasi wa Kristo. (Warumi 12:2)


Hata hivyo, mwito wetu unabaki uleule: kuwa mashahidi wa kweli wa Yesu kwa upendo na uaminifu, pasipo kujitenga au kuhukumu. Tunaitwa kumfuata Kristo katika dunia Isiyojali Ukristo kama chemchemi ya matumaini na si kama sauti za shutuma. (Mathayo 5:14–16)


N. T. Wright anasisitiza kuwa kwa sababu Yesu alifufuka kutoka kwa wafu, mpangilio mpya wa Mungu tayari umeanza kuonekana waziwazi ndani ya ulimwengu huu wa sasa. Hii ina maana kuwa kazi ya waamini si kuikimbia dunia, bali ni kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa na sasa – tukileta dalili hai za tumaini la uumbaji mpya hata katika mazingira ya ukinzani au ubaridi wa kiroho.


Katika hali hii ya giza na mabadiliko ya maadili, Biblia haituachi bila mifano. Hebu tuangalie baadhi ya mashujaa wa imani walioishi uaminifu usioyumba katikati ya mazingira magumu.



🔥 Mifano ya Kibiblia ya Uaminifu Usioyumba


  • Danieli Babeli – Aliishi kwa hekima, bila kuogopa kujitofautisha. (Danieli 1:8–21) .Danieli hakufuata mkondo wa jamii ya kipagani ya Babeli bali alisimama na msimamo wa kiimani, akitufundisha kuwa hekima ya kweli huambatana na hofu ya Mungu. Hata katika mazingira ya ugenini, uaminifu kwa Mungu huweza kung'aa na kuwa ushuhuda.


  • Mitume mbele ya Sanhedrini – Waliendelea kuhubiri hata walipokemewa. (Matendo 5:27–42) Kumtii Mungu kuliko wanadamu kulikuwa si chaguo la kiitikadi bali sharti la kiroho lililojengwa juu ya ushuhuda wa Kristo mfufuka. Walikumbatia mateso kama sehemu ya kuitwa kuwa mashahidi wa ukweli, wakionesha kuwa ushuhuda halisi huandamana na ujasiri wa kiroho.


  • Kanisa la kwanza chini ya mateso – Petro aliwatia moyo washiriki mateso ya Kristo. (1 Petro 4:12–16) Mateso kwa ajili ya Kristo si laana bali ni neema ya kushiriki katika utukufu wa Bwana. Waamini wanaitwa kuwa sehemu ya hadithi ya msalaba na ushindi wa ufufuo.


Haya si tu hadithi za zamani, bali ni miito halisi ya kuishi kama watoto wa nuru katika giza nene.

Hata hivyo, njia ya ufuasi haiko wazi daima. Kuna mitazamo mbalimbali inayoshindana, ambayo hujaribu kutafsiri au kupotosha maana ya kumfuata Kristo kwa kweli.



⚔️ Mitazamo Tofauti ya Namna ya Kumfuata Kristo


  1. Kujitenga – Kuishi katika "ngome" za Kikristo. Kujitenga kunaweza kuwalinda waamini dhidi ya uchafu wa kidunia, lakini huwazuia kutenda kazi ya Kristo ya kuangaza nuru yake mahali penye giza. (Mathayo 5:13–16)

  2. Upatanisho Usio na Msimamo – Injili laini, hakuna toba, hakuna msalaba. Injili inayopungukiwa na ukweli wa toba hupoteza nguvu yake ya kuleta mabadiliko ya kweli, ikigeuka kuwa ujumbe wa faraja badala ya wokovu. (Warumi 12:2)

  3. Ushupavu wa Kisiasa – Ufalme wa Mungu haujengi kwa mamlaka ya dunia bali kwa njia ya kujitoa na mateso, ambapo msalaba wa Yesu huwa njia ya ushindi wa kiroho. (Yohana 18:36)


Ni katika kukabiliana na mitazamo hiyo potofu ndipo tunahitaji kujenga azimio la kweli la maisha yanayoakisi Ufalme wa Mungu. Azimio hili haliko kwenye maneno matupu bali linaonekana kwenye mtindo wa maisha ya kila siku.



👑 Azimio la Uaminifu: Maisha Ya Kuakisi Ufalme Katika Dunia Iliyochanganyikiwa


🛡️ 1. Utambulisho wa Msalaba

Yesu hakutafuta umaarufu—alionyesha nguvu ya upendo wa kujitoa. Uaminifu huonekana kwenye unyenyekevu, upole, na huduma. (Wafilipi 2:5–11)


🌏 2. Ushiriki wa Kifalme

Sisi ni mabalozi wa Ufalme. Kama Yesu alivyoingia katika giza kwa upendo, nasi twaitwa kuangaza pasipo kujitenga. (2 Wakorintho 5:20; 1 Petro 2:11)


⏳ 3. Uaminifu Katika Mambo Madogo

Yesu alifundisha kuwa uaminifu katika mambo madogo ni msingi wa kuaminiwa kwa majukumu makubwa. Ufuasi wa kweli hujengwa katika uadilifu wa kila siku, hata katika yale yanayoonekana kuwa madogo mbele za watu. (Luka 16:10)


❤️ 4. Upendo Unaoshuhudia

Upendo si tu hoja ya kiroho, bali ni kielelezo hai cha jinsi Mungu alivyo kwa tabia na matendo—hasa kwa kuwapenda hata maadui (Mathayo 5:44), na kwa namna maisha ya waamini yaliyojaa bidii yalyoiwafanya mataifa kusema "wamegeuza dunia" (Matendo 17:6).


Kwa kufunga somo hili, tafakari hizi za kimaono zinatufunua mlango wa kuona uzuri wa msalaba kwa jicho la kiimani na tumaini la kina. Hapa tunaalikwa kuyaona maisha ya Kristo kama mfano wa mfalme ambaye alitawala kwa kujinyenyekeza.



🏆 Tafakari ya Kimaono: Njia ya Msalaba, Njia ya Mfalme


  • Nguvu Katika Udhaifu – Neema ya Kristo inaangaza katika udhaifu wetu. Hapo ndipo nguvu ya Mungu hujidhihirisha wazi zaidi—si kwa fahari ya kibinadamu bali kwa moyo uliopondeka unaomtegemea Bwana kwa kila pumzi. (2 Wakorintho 12:9–10)

  • Uzima Kupitia Kifo – Tunazikwa pamoja naye, tufufuliwe pia. Mauti haikuwa mwisho bali mlango wa uzima mpya; ndani ya ubatizo tunashiriki hadithi ya msalaba na tumaini la ufufuo. (Warumi 6:5–11)

  • Mfalme wa Msalaba – Heri maskini wa roho, kwao ni Ufalme wa Mbinguni. (Mathayo 5:3–12) Ufalme wa Mungu haujajengwa juu ya nguvu za kisiasa, bali juu ya mioyo iliyopondeka na mioyo ya wale wanaolilia haki.

  • Tumaini la Uumbaji Mpya – Sauti ya Yesu yaita: "Tazama, nayafanya yote kuwa mapya"—tangazo la mwanzo mpya ambapo machozi hubadilishwa kuwa tumaini na dunia huvaa uzuri wa milele. (Ufunuo 21:1–5)

Kama Israeli kule Babeli, tusingoje kurudi tu, bali tujenge hapa na sasa kwa upendo. (Yeremia 29:7)



🙏 Hitimisho: Kumfuata Kristo Katika Dunia Isiyojali Ukristo


Kumfuata Yesu si jambo la kidini tu, bali ni maisha halisi yenye thamani kubwa. Ni njia ya msamaha, matumaini, na upendo wa kweli.


📝 Maswali ya Kutafakari:

  • Kwa upande wako, kubeba msalaba wako kila siku kunamaanisha nini?

  • Ni hatua gani unaweza kuchukua kuonyesha Ufalme wa Mungu kazini au nyumbani?

  • Maisha ya Yesu yanapingana vipi na yale yanayopigiwa debe mitandaoni au kwenye vyombo vya habari?


🙌 Ombi la Baraka na Mwaliko wa Uitikio


Ee Bwana wa utukufu na rehema, utufundishe kutembea njia ya msalaba kwa uaminifu. Tujalie neema ya kuishi kila siku kama mashahidi wa Ufalme wako, tukitenda haki, tukipenda huruma, na kutembea kwa unyenyekevu pamoja nawe. Tunapobeba misalaba yetu kila siku, tujalie nguvu ya Roho Mtakatifu itusaidie kupendekeza jina lako kwa maneno na matendo.


Bwana akubariki na kukulinda. Bwana akuangazie uso wake na kukufadhili. Bwana akuinulie uso wake na kukupa amani. (Hesabu 6:24–26)


Mwaliko: Ni wapi maisha yako yanahitaji kuakisi njia ya msalaba zaidi? Andika sala fupi au wazo moja la utekelezaji kwa wiki hii, na mshirikishe rafiki au kikundi cha ushirika.


📚 Rasilimali Zilizopendekezwa kwa Kujifunza Zaidi


  • Following Jesus – N. T. Wright: Kitabu hiki kinaeleza kwa undani tabia na maono ya Yesu, kikifafanua maisha ya ufuasi kama kushiriki katika hadithi ya mabadiliko ya dunia kwa njia ya msalaba na upendo wa kujitoa.

  • Simply Jesus – N. T. Wright: Hapa Wright anafungua picha kamili ya Yesu kama Mfalme wa kweli wa Israeli, akieleza kwa nini kazi ya Yesu haipaswi kutengwa na mazingira ya kisiasa, ya kidini, na ya kibinadamu ya wakati wake.

  • God Crucified – Richard Bauckham: Bauckham anafafanua mafundisho ya Agano Jipya juu ya utambulisho wa Yesu kama Mungu, akionyesha jinsi msalaba ulivyokuwa sehemu ya utukufu wa Mungu mewe.weny

  • Jesus and the Forces of Death – Matthew Thiessen: Kitabu hiki kinaangazia jinsi Yesu alivyoingilia na kuvunja nguvu za uchafu na kifo katika huduma yake, akileta utakaso na uhai kama dalili za kuja kwa Ufalme wa Mungu.


Comments

Rated 0 out of 5 stars.
No ratings yet

Add a rating*
Image of a white top mauntain standing behind savana plain showing the wisdom of Creator God

Tutumie ujumbe,

nasi tutakujibu punde.

An image of Pr Enos Mwakalindile who is the author of this site
An image of a tree with a cross in the middle anan image of a tree with a cross in the middleaisha Kamili"

Unafurahia huduma hii ya Neno la Mungu bila kulipa chochote kwa sababu wasomaji kama wewe wameitegemeza kwa sala na sadaka zao. Tunakukaribisha kushiriki mbaraka huu kupitia namba +255 656 588 717 (Enos Enock Mwakalindile).

bottom of page