Uchambuzi wa Ayubu 22: Mashtaka Yanapotolewa Ili Kulinda Mfumo
- Pr Enos Mwakalindile
- 1 hour ago
- 15 min read
Elifazi Anapogeuka Kutoka Mfariji Kuwa Mwendesha Mashtaka, na Maneno ya Kweli Yanapotua Mahali Pasipofaa

Kuna wakati mfumo unapokuwa hatarini, na mwenye mfumo anaanza kutafuta dhambi itakayouokoa. Elifazi ameshindwa kuthibitisha kwamba waovu huanguka daima na wenye haki hustawi daima. Ayubu ameonyesha ulimwengu wenye nyumba za waovu zilizo salama, watoto wanaocheza, na makaburi yanayoheshimiwa. Sasa Elifazi hafungui moyo wake kwa ushahidi huo; anafungua jalada la mashtaka. Anasema Ayubu amewavua maskini nguo, amemnyima mchovu maji, amemfukuza mjane mikono mitupu, na ameiponda mikono ya yatima. Maandishi hayajatoa ushahidi wowote wa mambo hayo. Mfumo unaposhindwa kueleza jeraha, Elifazi analifanya jeraha kuwa ushahidi wa dhambi. Hata hivyo, ndani ya hotuba yake kali kuna maneno yenye uzuri: “Patanishwa na Mungu, uwe na amani.” Tatizo si kwamba kila neno lake ni la uongo. Tatizo ni kwamba dawa ya kweli amepewa mtu ambaye hana ugonjwa anaoshutumiwa kuwa nao.
1.0 Utangulizi: Mfariji Anapokaa Katika Kiti cha Mwendesha Mashtaka
Mwanzoni, Elifazi hakuwa hivi.
Katika hotuba yake ya kwanza, alimkumbusha Ayubu jinsi alivyowahi kuwafundisha wengi, kuimarisha mikono iliyolegea, na kuwatia nguvu waliokuwa wanajikwaa (4:3–4). Ingawa tayari aliamini mateso yanahusiana na kosa fulani, bado alizungumza kama rafiki mwenye tumaini kwamba nidhamu ya Mungu ingeweza kuzaa uponyaji.
Lakini mazungumzo yamekuwa marefu. Ayubu hajakubali kuwa mwovu. Hajatoa ungamo ambalo rafiki zake wamelisubiri. Ameendelea kusema kwamba mateso yake hayalingani na maisha aliyoishi. Zaidi ya hayo, katika sura ya 21, ametoa ushahidi unaotikisa mfumo wao: waovu huweza kuishi muda mrefu, kuona watoto wao wakistawi, kufurahia muziki, kumkataa Mungu, kufa kwa amani, na kuzikwa kwa heshima.
Elifazi sasa anasimama katika njia panda. Anaweza kukubali kwamba ulimwengu ni wenye fumbo zaidi kuliko alivyodhani. Anaweza kurudi kuketi karibu na rafiki yake na kusema, “Sielewi, lakini sitakuacha.” Au anaweza kuilinda theolojia yake kwa kuongeza uzito wa mashtaka.
Anachagua mashtaka.
Ayubu 22 ni hotuba ya tatu na ya mwisho ya Elifazi. Inaanza kwa maswali kuhusu ikiwa mwanadamu anaweza kumfaidia Mungu. Kisha sauti inabadilika ghafla: “Je, uovu wako si mkuu? Maovu yako hayana mwisho” (22:5). Kutoka hapo Elifazi anataja dhambi maalumu kana kwamba alikuwa shahidi: Ayubu amechukua dhamana bila sababu, amewavua watu nguo, amemnyima mchovu maji, amemnyima mwenye njaa chakula, amewafukuza wajane, na ameponda nguvu za yatima (22:6–9).
Lakini msomaji anajua jambo ambalo Elifazi hajui—au hataki kulikubali. Mungu mwenyewe alimweleza Ayubu kuwa mtu mkamilifu na mnyofu, anayemcha Mungu na kujiepusha na uovu (1:1, 8; 2:3). Hakuna tukio katika simulizi linalothibitisha mashtaka haya. Baadaye Ayubu ataeleza kwamba aliwaokoa maskini waliolia, aliwasaidia yatima, aliufurahisha moyo wa mjane, na akawa macho kwa kipofu na miguu kwa kilema (29:12–16). Katika sura ya 31, ataikana moja kwa moja orodha ya dhambi ambazo Elifazi sasa anamtwisha (31:16–23).
Kwa hiyo, Ayubu 22 inatufikisha kwenye eneo la hatari sana la kitheolojia: Mtu anapopenda maelezo yake kuliko mwanadamu aliye mbele yake, anaweza kuanza kutunga hatia ili kulinda mfumo wake.
Lakini sura hii ina fumbo jingine. Nusu yake ya mwisho ina maneno mazuri kuhusu kurudi kwa Mungu, kulihifadhi neno lake moyoni, kumfanya Mwenyezi kuwa hazina, kuinua uso katika maombi, kutembea katika nuru, na kuwaombea wengine. Maneno yahengayenga yana ukweli. Tatizo lake ni mahali yanapotua. Elifazi anamwita mwenye haki atubu dhambi ambazo hajazitenda.
Hivyo Ayubu 22 inauliza swali la kichungaji lenye makali:
Je, hata maneno matakatifu yanaweza kuwa silaha yanapotolewa bila kusikiliza, bila ushahidi, na bila upendo?
2.0 Muktadha wa Kihistoria na Kifasihi: Hotuba ya Mwisho ya Elifazi
Ayubu 22 inafungua kile ambacho mara nyingi huiitwa mzunguko wa tatu wa majadiliano. Mzunguko huu ni mfupi, umevurugika zaidi katika muundo wake, na unaonyesha kwamba mazungumzo yamefika ukingoni. Elifazi anazungumza katika sura ya 22; Ayubu anajibu kwa hotuba ndefu katika sura ya 23–24; hotuba ya Bildadi katika sura ya 25 ni fupi sana; na Sofari hatapewa hotuba nyingine iliyo wazi.
Maneno yameanza kuishiwa nguvu, lakini ukali wake unaongezeka.
Hotuba ya Elifazi ina sehemu tatu kuu:
Mashtaka dhidi ya Ayubu (22:1–11). Elifazi anaanza kwa kusema kwamba haki ya mwanadamu haimwongezei Mungu chochote. Kisha anahitimisha kwamba mateso ya Ayubu lazima yatokane na uovu wake mkubwa. Anaorodhesha madai ya unyanyasaji wa maskini, wajane, na yatima.
Mabishano kuhusu namna Mungu anavyohusika na mambo ya wanadamu (22:12–20). Elifazi anadai kwamba Ayubu anamwona Mungu kuwa mbali mno, amefichwa na mawingu, na hawezi kuona yanayotokea duniani. Kisha anamrudisha kwenye “njia ya zamani” ya waovu waliokumbwa na gharika na moto.
Wito wa kutubu na kurejeshwa (22:21–30). Elifazi anamwita Ayubu apatanishwe na Mungu, alihifadhi neno lake moyoni, aondoe uovu katika hema yake, aweke dhahabu mavumbini, na amfanye Mwenyezi kuwa hazina yake. Anaahidi amani, maombi yanayosikiwa, nuru njiani, na nguvu ya kuwaombea wengine.
Muundo huo unaonyesha jinsi Elifazi anavyofikiri. Kwanza anatengeneza utambuzi wa ugonjwa: Ayubu ni mwovu. Kisha anaeleza theolojia inayothibitisha utambuzi huo: Mungu huwaangamiza waovu. Hatimaye anatoa tiba: Ayubu na atubu, ndipo atarejeshwa.
Ikiwa hatua ya kwanza ingekuwa sahihi, mengi katika hatua ya tatu yangekuwa ushauri wenye nguvu. Lakini utambuzi wake ni wa uongo. Kwa hiyo, hata dawa nzuri inageuka kuwa mzigo.
Kuna kejeli muhimu katika aya ya 6. Elifazi anasema Ayubu amechukua dhamana ya ndugu yake “bila sababu.” Kauli hiyo inarudisha mwangwi wa dibaji ya kitabu. Mshitaki aliuliza kama Ayubu anamcha Mungu “bure,” yaani bila sababu au bila malipo (1:9). Baadaye Mungu alimwambia Mshitaki kwamba alikuwa amemchochea dhidi ya Ayubu ili amwangamize “bila sababu” (2:3). Ukweli ni kwamba mateso ya Ayubu hayajasababishwa na dhambi anazodai Elifazi. Lakini sasa Elifazi anachukua maneno ya “bila sababu” na kuyageuza kuwa shtaka dhidi ya Ayubu.
Hapo ndipo msomaji anaona umbali kati ya maarifa ya mbinguni na hitimisho la rafiki zake. Elifazi anadhani mateso makubwa yanahitaji dhambi kubwa. Dibaji imetufundisha kwamba hitimisho hilo si sahihi.
Ayubu 22 kwa hiyo si hotuba ya mtu asiyejua kitu chochote kuhusu Mungu. Ni hotuba ya mtu mwenye kweli nyingi, lakini ambaye mfumo wake umekuwa mgumu kiasi cha kumzuia kumwona mtu aliye mbele yake.
3.0 Kutembea Ndani ya Andiko: Kutoka Maswali ya Hekima Hadi Ahadi Iliyowekwa Mahali Pasipofaa
3.1 “Je, Mwanadamu Aweza Kumfaidia Mungu?” — Ukweli Unapogeuzwa Kuwa Shtaka (22:1–5)
Elifazi anaanza kwa maswali:
Je, mwanadamu anaweza kuwa na faida kwa Mungu?
Je, Mwenyezi hupata kitu kwa sababu mtu ni mwenye haki?
Je, Mungu huongezewa mali kwa sababu njia za mwanadamu hazina lawama? (22:2–3).
Katika kiwango fulani, jibu ni la wazi. Mungu si mwajiri anayehitaji kazi yetu ili biashara yake iendelee. Hatuwezi kumfanya Mungu awe tajiri zaidi, mwenye hekima zaidi, au kamili zaidi. Utii wetu haumweki katika deni letu. Uumbaji wote tayari ni wake. Haki ya mwanadamu haiwezi kuwa sarafu ya kumnunulia Mungu.
Lakini Elifazi anatumia ukweli huo kwa njia isiyo sahihi.
Anadhani Ayubu anapodai kuwa mwadilifu, anajaribu kumweka Mungu katika deni lake. Lakini Ayubu hasemi kwamba amemfaidia Mungu na sasa anadai malipo. Anasema tu kwamba mashtaka ya rafiki zake si ya kweli. Anatamani Mungu asikilize kesi yake na kuthibitisha ukweli.
Kisha hoja ya Elifazi inageuka kwa kasi. Anauliza kama Mungu anamkemea Ayubu kwa sababu ya kumcha Mungu (22:4). Kwa maoni yake, jambo hilo haliwezekani kabisa. Ikiwa Mungu ameingia katika hukumu na Ayubu, lazima sababu iwe upande wa Ayubu. Ndipo anatoa hitimisho: “Je, uovu wako si mkuu? Wala maovu yako hayana mwisho?” (22:5).
Angalia kilichotokea. Elifazi hana ushahidi mpya. Hana shahidi. Hana tukio. Ana mateso ya Ayubu na mfumo unaosema mateso hayo lazima yawe adhabu. Kwa hiyo, ukali wa mateso unakuwa kipimo cha ukubwa wa dhambi.
Hii ndiyo mantiki hatari inayoweza kujificha ndani ya dini: “Kwa kuwa jambo baya sana limekupata, lazima uwe umefanya jambo baya sana.” Ayubu anakataa mantiki hiyo, na dibaji ya kitabu tayari imemthibitisha.
Ni kweli kwamba Mungu hatudaiwi. Lakini ni kweli pia kwamba Mungu anajali uadilifu wa viumbe wake, husikia kilio cha aliyeonewa, na hapendezwi na ushuhuda wa uongo. Utukufu wa Mungu haulindwi kwa kumfanya asiye na hatia kuwa mwenye hatia.
Ukweli kuhusu ukuu wa Mungu unapotumiwa kufuta ukweli kuhusu jirani, umeacha kuwa hekima na umegeuka kuwa silaha.

3.2 “Umemnyima Mwenye Njaa Chakula” — Dhambi Zinazotungwa Kutokana na Jeraha (22:6–9)
Sasa Elifazi anakuwa mahususi.
Anamshutumu Ayubu kwa kuchukua dhamana kutoka kwa ndugu zake bila sababu na kuwavua watu mavazi yao (22:6). Katika ulimwengu wa kale, mtu maskini angeweza kutoa vazi lake kuwa dhamana ya deni. Lakini sheria ya Israeli baadaye ingesisitiza kwamba vazi hilo lirudishwe kabla ya usiku, kwa sababu ndilo blanketi la maskini wakati wa baridi (Kutoka 22:26–27; Kumbukumbu la Torati 24:10–13). Kulichukua bila huruma ilikuwa kuitumia nguvu ya kiuchumi kuuvua utu wa maskini.
Elifazi anaendelea: Ayubu hakumpa maji aliyechoka na alimnyima mwenye njaa chakula (22:7). Maji na mkate ni zawadi za msingi kabisa za ukarimu. Kumnyima mchovu maji katika nchi kavu si ukosefu mdogo wa adabu; ni kuuchezea uhai wake.
Aya ya 8 inaonyesha ulimwengu ambao mwenye nguvu anajifanya mmiliki wa nchi na mtu mwenye cheo ndiye anayeruhusiwa kuishi humo. Huenda Elifazi anamshutumu Ayubu kwa kutumia hadhi yake kuchukua ardhi au kwa kuamini kwamba dunia ni mali ya wenye mamlaka. Kwa njia yoyote, picha ni ya nguvu inayojilinda na kuwafukuza wanyonge.
Kisha mashtaka yanafika kwa wajane na yatima: “Umewafukuza wajane mikono mitupu, na mikono ya yatima imevunjwa” (22:9). Katika Biblia, wajane na yatima husimama kama alama ya wale wasiokuwa na mlinzi wa kijamii. Mungu hujitambulisha kama mtetezi wao (Kumbukumbu la Torati 10:18; Zaburi 68:5). Kuwadhulumu ni kushambulia eneo ambalo haki ya Mungu hulilinda kwa namna ya pekee.
Dhambi hizi ni halisi. Ni nzito. Zinapaswa kuitwa kwa majina yao katika kila kizazi: mikopo inayowavua maskini, mifumo inayokusanya ardhi mikononi mwa wenye nguvu, kunyimwa kwa mahitaji ya msingi, kufukuzwa kwa wajane, na kuvunjwa kwa nguvu za watoto wasio na watetezi.
Tatizo si kwamba Elifazi anachukia dhambi zisizokuwapo duniani. Tatizo ni kwamba anamtwisha Ayubu dhambi hizo bila ushahidi.
Na maandishi baadaye yataonyesha kinyume chake. Ayubu atasema: “Nilimwokoa maskini aliyelia, na yatima asiye na mtu wa kumsaidia. Moyo wa mjane niliufanya uimbe kwa furaha” (29:12–13). Alikuwa macho kwa kipofu, miguu kwa kilema, na baba kwa maskini (29:15–16). Atajiweka chini ya hukumu ikiwa aliwahi kumnyima maskini alichotamani au kuufanya moyo wa mjane uzimie (31:16–23).
Elifazi anamchora Ayubu kwa rangi zinazopingana na maisha yake.
Hili ni onyo la kudumu. Tuhuma maalumu zinahitaji ushahidi maalumu. Hatuwezi kutumia hali ya mtu, uvumi, cheo chake, au mfumo wetu wa kidini kuwa mbadala wa ukweli.
Kupinga udhalimu ni haki; kumbandika asiye na hatia udhalimu ambao hajautenda ni udhalimu mwingine.
3.3 “Kwa Sababu Hiyo Mitego Imekuzunguka” — Maumivu Yanapogeuzwa Kuwa Ushahidi (22:10–11)
Baada ya kuorodhesha mashtaka, Elifazi anatafsiri mateso ya Ayubu: “Kwa sababu hiyo mitego imekuzunguka, na hofu ya ghafla inakutisha” (22:10).
Maneno “kwa sababu hiyo” ndiyo bawaba ya hoja yake. Kwa sababu Ayubu amewadhulumu maskini—ndiyo maana mitego imemnasa. Kwa sababu aliwanyima wenye njaa chakula—ndiyo maana hofu imemshika. Kwa sababu aliwafukuza wajane—ndiyo maana giza limemfunika. Kwa sababu aliiponda mikono ya yatima—ndiyo maana mafuriko yamemzidi (22:11).
Lakini Elifazi amepanga mfuatano kwa kuanzia mwisho. Anaona maumivu, kisha anarudi nyuma na kutunga kosa linaloweza kuyaeleza. Mateso hayafuati ushahidi wa dhambi; mashtaka yanafuata ushahidi wa mateso.
Picha anazotumia ni za nguvu. Mitego inazunguka njia. Hofu inatokea ghafula. Giza linazuia kuona. Maji mengi yanapanda na kufunika kila kitu. Hizo ni picha zinazofanana na uzoefu ambao Ayubu mwenyewe ameueleza. Lakini badala ya kuingia ndani ya picha hizo na kukaa na rafiki yake, Elifazi anazitumia kama vielelezo vya hukumu.
Wakati mwingine anayeteseka husema, “Ninahisi nimezama,” halafu mfariji anajibu, “Basi lazima kuna dhambi iliyokuvuta majini.” Hapo lugha ya maombolezo imegeuzwa kuwa ushahidi wa mashtaka.
Biblia inajua kwamba dhambi inaweza kuwa na matokeo. Haitenganishi kabisa matendo na mavuno yake. Lakini kitabu cha Ayubu kinatukataza kugeuza kanuni hiyo kuwa mashine ya kueleza kila jeraha. Si kila mtego ni adhabu. Si kila giza ni hukumu. Si kila mafuriko yanafunua kosa la siri.
Msalaba unasimama kama ushahidi mkuu. Yesu anazungukwa na mitego, anaingia katika giza, na maji ya kifo yanamfunika—lakini si kwa sababu yeye ni mwovu. Mwenye haki anaingia kwenye kina ambacho mfumo wa Elifazi usingeweza kueleza.
Maumivu yanahitaji huruma kabla hayajageuzwa kuwa hoja.

3.4 “Mawingu Mazito Humficha” — Maombolezo Yanapotafsiriwa Kuwa Uasi (22:12–14)
Elifazi sasa anamtazama Mungu aliye juu kuliko nyota. “Je, Mungu hayuko katika kimo cha mbingu? Tazama kilele cha nyota, jinsi kilivyo juu!” (22:12). Hapo anatumia lugha ya sifa. Mungu ametukuka. Anautawala ulimwengu kutoka juu.
Lakini kisha Elifazi anamwekea Ayubu maneno mdomoni: “Unasema, Mungu anajua nini? Je, anaweza kuhukumu kupitia giza nene? Mawingu mazito humficha asiweze kuona, naye hutembea juu ya duara la mbingu” (22:13–14).
Kwa maoni ya Elifazi, Ayubu anaamini Mungu yuko mbali sana kiasi kwamba haoni mambo ya duniani. Hilo lingemfanya Ayubu afanane na waovu wanaodhani wanaweza kutenda bila kuonekana.
Lakini hayo si malalamiko ya Ayubu.
Ayubu hajawahi kusema kwamba Mungu haoni. Kwa kweli, mara nyingi amelia kwa sababu Mungu anaonekana kumwangalia kwa ukaribu usiovumilika: “Mwanadamu ni nini hata umtukuze, na kumwangalia kila asubuhi?” (7:17–18). Amesema kwamba akitenda dhambi, Mungu humwona na hamwachi (10:14). Tatizo lake si kwamba Mungu haoni; ni kwamba haelewi kwa nini Mungu anayaona mateso na bado hamtetei.
Elifazi anachukua swali la Ayubu kuhusu haki na kuligeuza kuwa kukana maarifa ya Mungu. Anachukua maombolezo na kulipa jina la uzushi.
Hili hutokea mara nyingi katika jumuiya za imani. Mtu anapouliza, “Mungu alikuwa wapi?” tunaweza kusikia kana kwamba amesema, “Mungu hayupo.” Mtu anaposema, “Sioni haki,” tunaweza kumjibu kana kwamba amesema, “Mungu si mwenye haki.” Lakini maombolezo ya Biblia si uasi wa lazima. Mara nyingi ni imani inayomtafuta Mungu kwa nguvu kwa sababu bado inaamini anapaswa kusikia.
Zaburi zimejaa maswali ya namna hiyo. Manabii wanalia. Yesu mwenyewe anauliza, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” (Mathayo 27:46). Swali hilo halimfanyi asiwe mwaminifu. Linaonyesha kina cha utii wake ndani ya giza.
Usimwite mtu asiyeamini kwa sababu tu imani yake inaongea kwa sauti ya maumivu.
3.5 “Je, Utaishika Njia ya Kale?” — Elifazi Anarudisha Hoja ya Waovu (22:15–20)
Elifazi anamuuliza Ayubu kama ataendelea katika njia ya zamani iliyokanyagwa na waovu (22:15). Anawaeleza watu waliokatiliwa mbali kabla ya wakati wao, msingi wao ukichukuliwa na mafuriko (22:16). Picha inaweza kuamsha kumbukumbu ya gharika ya siku za Nuhu—ulimwengu wa jeuri uliofagiliwa na maji (Mwanzo 6–7).
Watu hao walimwambia Mungu, “Tuondokee,” na wakauliza, “Mwenyezi anaweza kutufanyia nini?” (22:17). Haya ni karibu maneno yale yale ambayo Ayubu ameyanukuu katika sura ya 21. Elifazi sasa anayachukua na kuyarudisha dhidi yake.
Anakubali kwamba Mungu alijaza nyumba zao vitu vizuri, lakini anasisitiza mwisho wao ulikuwa uharibifu. Kisha anarudia kauli ya Ayubu: “Shauri la waovu na liwe mbali nami” (22:18; linganisha 21:16). Ni kana kwamba anasema, “Ayubu, maneno yako mwenyewe yanaunga mkono hoja yangu. Waovu wanaweza kustawi kwa muda, lakini mafuriko na moto vitawamaliza.”
Wenye haki wanapoona anguko lao, Elifazi anasema, hufurahi; wasio na hatia huwacheka (22:19). Wanatazama mali ya waovu ikikatiliwa mbali na utajiri wao ukiliwa na moto (22:20).
Katika sehemu hii, Elifazi anarekebisha madai yake kiasi. Anakubali kile Ayubu alichosema kuhusu nyumba za waovu kujazwa mema, lakini bado anasisitiza kwamba mwisho unaoonekana wa hukumu lazima uje. Hata hivyo, hakabiliani kikamilifu na hoja ya Ayubu kwamba baadhi yao hufa kwa amani na kuzikwa kwa heshima. Badala yake, anarudi kwenye picha za jadi za gharika na moto.
Kuna pia jambo la kusumbua katika furaha ya wenye haki juu ya uharibifu. Biblia inajua shangwe ya kuona ukandamizaji ukikomeshwa; ukombozi wa wahanga una sababu ya kuimba. Lakini hekima nyingine ya Biblia inaonya: “Adui yako aangukapo, usifurahi” (Mithali 24:17). Haki ya Mungu haipaswi kuzaa moyo unaopenda kuona watu wakiteketea.
Elifazi amekuwa na hamu kubwa ya kuona mfumo wake ukithibitishwa kuliko kuona rafiki yake akiponywa. Anguko la mwovu limemvutia zaidi kuliko kilio cha mtesekaji.
Haki ya kweli hufurahia ukombozi wa walioonewa; hailishi roho kwa kutazama maangamizi.

4.0 Tafakari ya Kitheolojia: Kumtetea Mungu Bila Kumsingizia Mwanadamu
Ayubu 22 inatufundisha kwamba si kila utetezi wa Mungu unaomtukuza Mungu.
Elifazi anafikiri analinda haki ya Mwenyezi. Hawezi kukubali kwamba Ayubu ni mwenye haki na bado anateseka, kwa sababu jambo hilo lingeutikisa mfumo wake wa namna Mungu anavyotawala. Kwa hiyo, ili Mungu aendelee kuonekana mwenye haki ndani ya mfumo huo, Ayubu lazima awe mwovu. Elifazi anamchafua mwanadamu ili kuitunza picha yake ya Mungu.
Lakini mwanadamu huyo ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Ushuhuda wa uongo dhidi yake hauwezi kuwa ibada. Huwezi kumtukuza Muumba kwa kumsingizia kiumbe wake.
Kwanza, sura hii inatofautisha kati ya theolojia ya kweli na matumizi ya kweli ya theolojia. Mungu hatudaiwi. Toba ni muhimu. Neno la Mungu linapaswa kuhifadhiwa moyoni. Mali haipaswi kuchukua nafasi ya Mungu. Mungu anapaswa kuwa hazina yetu. Maombi na maombezi ni zawadi za agano. Mambo hayo yana ukweli. Lakini yakitumika kumlazimisha asiye na hatia akiri dhambi ambayo hakutenda, yamewekwa mahali pasipofaa.
Pili, Ayubu 22 inafunua kwamba wito wa kutubu unahitaji ukweli, si dhana. Biblia haitufundishi kunyamaza mbele ya dhambi halisi. Elifazi anataja maovu ambayo Mungu anayachukia: unyonyaji wa kiuchumi, kunyimwa kwa maji na mkate, ubinafsi wa wenye ardhi, na kupondwa kwa wajane na yatima. Kanisa lazima liyataje maovu hayo. Lakini haki haiwezi kujengwa juu ya shtaka lisilo na ushahidi. Toba ya kweli inaanza pale ukweli wa kweli unaposemwa.
Tatu, sura hii inatufundisha kwamba maombolezo si sawa na kumwacha Mungu. Elifazi anamsikia Ayubu akilalamika kuhusu ukimya wa Mungu na anahitimisha kwamba Ayubu anaamini Mungu haoni. Lakini Ayubu analalamika kwa Mungu kwa sababu bado anamchukulia Mungu kwa uzito. Imani iliyojeruhiwa inaweza kuuliza maswali makali bila kukata mizizi yake. Mungu wa Biblia ni mkuu kiasi cha kupokea kilio kisichopangiliwa vizuri.
Nne, mwisho wa hotuba unaonyesha nguvu ya maombezi yanayogeuza adui kuwa jirani. Elifazi anaahidi kwamba Ayubu ataweza kuwaokoa wengine kwa usafi wa mikono yake. Mwisho wa kitabu, Ayubu atawaombea watu waliomvunja kwa maneno. Rehema yake haitasema mashtaka yao yalikuwa sahihi. Itasema kwamba neema inaweza kupita hata katika moyo ulioumizwa bila kuuita uovu kuwa wema.
Hapo Ayubu anakuwa ishara ndogo inayotuelekeza kwa Kristo. Yesu ndiye mwenye haki anayeshtakiwa kwa uongo, anayebeba hukumu ya wengine, na anayesimama akiwa Mwombezi. Katika yeye, wito wa Elifazi wa “kupatanishwa na Mungu” unapata msingi wake wa kweli. Amani na Mungu haiji kwa kutunga ungamo la uongo, wala kwa kununua kibali kwa dhahabu. Inakuja kwa neema kupitia Mwana mwaminifu ambaye anatuleta karibu (Warumi 5:1; 2 Wakorintho 5:18–21).
Msalaba pia unarekebisha namna tunavyowaita wengine watubu. Hatusimami juu yao kama waendesha mashtaka wanaotafuta kuthibitishwa. Tunasimama chini ya msalaba kama wenye dhambi waliopokea rehema. Tunataja dhambi kwa ukweli, lakini kwa machozi. Tunaita watu warudi kwa Mungu, lakini hatubuni hatia yao. Tunatamani kurejeshwa kwao, si ushindi wa mfumo wetu.
Mungu hahitaji uongo wetu ili aonekane mwenye haki. Msalaba na ufufuo vinatosha kuonyesha kwamba haki yake inaweza kupita katika njia ambazo mifumo yetu midogo haiwezi kuzichora.
5.0 Matumizi Maishani: Maneno Matakatifu Yanapohitaji Moyo wa Huruma
Ayubu 22 inatoa hekima ya vitendo kwa wachungaji, walimu, washauri, familia, na jumuiya za imani.
Kwanza, usibuni dhambi ili kueleza mateso. Ikiwa huna ushahidi, usijaze pengo kwa tuhuma. Ugonjwa, kufilisika, msiba wa familia, kukataliwa, au kupoteza kazi havithibitishi kosa la siri. Ukweli hauhitaji ubashiri wenye mavazi ya kiroho.
Pili, tenganisha kanuni nzuri na matumizi yake. Kauli inaweza kuwa sahihi na bado isiwe jibu sahihi kwa mtu aliye mbele yako. Kabla ya kunukuu andiko, uliza: Je, nimemsikiliza? Je, andiko hili linalenga hali yake kweli? Je, maneno yangu yatamleta karibu na Mungu au yataongeza jeraha lisilo lake?
Tatu, chukua mashtaka ya udhalimu kwa uzito—lakini pia chukua ushahidi kwa uzito. Kuwadhulumu maskini, wajane, na yatima ni dhambi kubwa. Usinyamazishe wahanga. Wakati huohuo, usiharibu jina la mtu kwa uvumi au hitimisho lililotokana na hali yake. Haki humlinda aliyeonewa na pia hukataa ushuhuda wa uongo.
Nne, usiite maombolezo uasi kwa haraka. Mtu anaweza kuuliza Mungu yuko wapi kwa sababu bado anamtamani. Sikiliza kilio kilicho chini ya swali. Wakati mwingine kauli inayoonekana kuwa ngumu ni sala inayopigania kuendelea kupumua.
Tano, usijaribu kumtetea Mungu kwa kumdhalilisha mwanadamu. Mungu si dhaifu kiasi cha kuhitaji tumsafishie jina kwa kumchafua mtesekaji. Mtetee Mungu kwa kusema ukweli, kutenda haki, kuonyesha rehema, na kukaa kwa uaminifu karibu na waliojeruhiwa.
6.0 Maswali ya Kutafakari
1. Elifazi anahama kwa namna gani kutoka maswali ya jumla kuhusu Mungu hadi madai kwamba uovu wa Ayubu hauna mwisho?
2. Kwa nini mashtaka ya Ayubu 22:6–9 ni mazito kimaadili, na kwa nini bado ni makosa kuyatumia dhidi ya Ayubu?
3. Maelezo ya Ayubu kuhusu maisha yake katika 29:12–16 na 31:16–23 yanapingana vipi na picha iliyochorwa na Elifazi?
4. Elifazi anayaelewaje vibaya malalamiko ya Ayubu kuhusu Mungu aliyejificha nyuma ya mawingu?
5. Ni kwa njia gani wito wa “kupatanishwa na Mungu” katika 22:21–30 ni wa kweli, lakini umewekwa mahali pasipofaa?
6. Kuna tofauti gani kati ya kuhubiri toba kwa upendo na kutumia toba kama njia ya kumshinda mtu katika mabishano?
7. Ahadi ya Elifazi kuhusu maombezi katika 22:29–30 inatimizwaje kwa kejeli katika Ayubu 42:7–10?
8. Yesu, aliyeshtakiwa kwa uongo na kuwaombea washtaki wake, anatubadilishiaje namna ya kusema na wanaoteseka?
7.0 Ombi la Kujibu
Ee Mungu wa kweli na rehema,
utusamehe tunapopenda majibu yetu
kuliko watu walioumbwa kwa mfano Wako.
Tusiruhusu mfumo wetu kuwa madhabahu
ambapo jina la asiye na hatia linatolewa sadaka.
Tufundishe kusikiliza kabla ya kushtaki,
kuchunguza kabla ya kuhitimisha,
na kulia pamoja na wanaolia
kabla ya kuwapa maelezo.
Unapotuonyesha udhalimu wa kweli,
tupe ujasiri wa kuutaja:
mkate ulionyimwa mwenye njaa,
maji aliyonyimwa mchovu,
mjane aliyefukuzwa,
na yatima aliyepondwa.
Lakini tulinde na ushuhuda wa uongo,
uvumi, na mashaka yanayovaa mavazi ya hekima.
Tufundishe kuyapokea maneno kutoka kinywani Mwako
na kuyaweka mioyoni mwetu.
Uwe hazina yetu kuliko dhahabu,
amani yetu ndani ya giza,
na nuru yetu wakati njia haionekani.
Tufanye watu wa toba,
lakini pia watu wa huruma.
Tufanye waombezi,
si waendesha mashtaka.
Na tunapojeruhiwa na maneno ya rafiki,
tupe neema ya kusimama katika ukweli
bila kuruhusu uchungu ututawale.
Tukumbushe Yesu Kristo,
Mwenye mikono safi aliyeshtakiwa kwa uongo,
aliyesulubiwa pamoja na wakosaji,
na anayetuombea akiwa hai.
Katika jina lake,
Mpatanishi wetu na Amani yetu.
Amina.
8.0 Dirisha la Kuangazia Kinachofuata: Ayubu Anapomtafuta Mungu Asiyeonekana
Elifazi amemwambia Ayubu, “Patanishwa na Mungu, uwe na amani. Rudi kwa Mwenyezi, nawe utajengwa.” Lakini katika Ayubu 23, tatizo la Ayubu litaonekana wazi: angependa kwenda kwa Mungu—lakini hamwoni.
Atasema, “Laiti ningejua mahali ninapoweza kumpata.” Atatafuta mbele na nyuma, kushoto na kulia, lakini Mungu ataonekana kutokuwapo (23:3, 8–9). Hata hivyo, ndani ya kutokuonekana huko, Ayubu atatoa ungamo lenye nguvu: “Yeye anaijua njia niendeayo; akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu” (23:10).
Elifazi amemwambia aitupe dhahabu mavumbini na kumfanya Mungu kuwa dhahabu yake. Ayubu atajibu kwa picha nyingine ya dhahabu: yeye mwenyewe yuko katika tanuru la fumbo, na anaamini kwamba Mungu, ingawa amejificha, anaijua njia yake.
Ayubu hatajibu kila shtaka moja baada ya jingine. Hatakubali ungamo la uongo ili kupata amani ya haraka. Atakwenda moja kwa moja kwenye mahakama ya Mungu, akitamani kuwasilisha kesi yake mbele ya Hakimu ambaye hawezi kumpata—lakini ambaye bado anaamini anamjua.
9.0 Bibliografia Iliyofafanuliwa
Alter, Robert. The Wisdom Books: Job, Proverbs, and Ecclesiastes—A Translation with Commentary. New York: W. W. Norton, 2010. Tafsiri yake inahifadhi mabadiliko makali ya sauti ya Elifazi, kutoka mabishano hadi mashtaka na kisha wito wa kurejeshwa.
Clines, David J. A. Job 21–37. Word Biblical Commentary 18A. Nashville: Thomas Nelson, 2006. Inatoa uchambuzi wa kina wa maswali ya Elifazi, tabia ya kimahakama ya mashtaka yake, changamoto za tafsiri katika aya ya 8 na 30, na mchanganyiko wa ukali na ahadi katika hotuba hii.
Crenshaw, James L. Old Testament Wisdom: An Introduction. Louisville: Westminster John Knox, 2010. Husaidia kuweka hotuba hii ndani ya mvutano mpana wa hekima kuhusu malipo, haki ya Mungu, na uzoefu wa mateso yasiyostahiliwa.
Habel, Norman C. The Book of Job: A Commentary. Old Testament Library. Philadelphia: Westminster, 1985. Hufafanua mikakati ya mabishano ya Elifazi na namna hotuba yake inavyotumia theolojia ya kawaida kumweka Ayubu upande wa waovu.
Hartley, John E. The Book of Job. New International Commentary on the Old Testament. Grand Rapids: Eerdmans, 1988. Inagawa Ayubu 22 katika mashtaka, mabishano kuhusu utendaji wa Mungu, na wito wa kutubu; pia inaonyesha hatari ya maneno ya kweli yanayotumiwa kutokana na mtazamo usio sahihi.
Newsom, Carol A. The Book of Job: A Contest of Moral Imaginations. Oxford: Oxford University Press, 2003. Husaidia kuelewa mazungumzo kama mgongano wa mitazamo ya kimaadili ambapo mfumo wa rafiki zake unazidi kushindwa kumpa nafasi mtesekaji asiye na hatia.
Walton, John H., and Tremper Longman III. How to Read Job. Downers Grove, IL: IVP Academic, 2015. Mwongozo wa kusoma hotuba za rafiki kwa uangalifu—ukitambua chembe za ukweli ndani yake bila kukubali matumizi yao potovu dhidi ya Ayubu.




Comments