Uchambuzi wa Esta 6: Usiku Usiolala wa Majalio ya Kimungu — Wakati Uaminifu Uliosahaulika Unapokumbukwa
- Pr Enos Mwakalindile
- 1 day ago
- 16 min read

Mti wa kunyongea ulisimama ukiwa tayari gizani. Hamani alifika mapema akiwa na sumu ya mauaji kinywani mwake. Lakini mfalme hakuweza kulala, kumbukumbu zilianza kunena, na usiku wenyewe ukawa mtumishi wa rehema iliyofichika.
1.0 Utangulizi: Usiku Unapokataa Kulala
Kuna majira ya usiku yanayoonekana tupu, lakini ndani yake Mungu anasogeza mambo kimya kimya. Wakati watu wamelala, mipango inaendelea. Wakati maadui wanapanga madhara, rehema huandaa majira yake. Wakati wenye haki wanaonekana kusahaulika, kumbukumbu fulani husubiri saa yake kuitwa.
Esta 6 ni bawaba ya Biblia nzima ya kitabu hiki. Mpaka hapa, simulizi imekuwa ikigeuzwa taratibu kuelekea hatarini. Hamani ameinuliwa. Mordekai amekataa kusujudu. Amri ya kifo dhidi ya Wayahudi imetolewa. Esta amehatarisha maisha yake na kumwalika mfalme pamoja na Hamani kwenye karamu mbili. Hamani amerudi nyumbani akiwa ameumizwa na msimamo thabiti wa Mordekai, kisha amechonga mti mrefu wa kumnyonga.
Kila kitu kinaonekana kiko tayari kwa kifo cha Mordekai. Lakini usiku ule, mfalme alikosa usingizi.
Sentensi hiyo ni tulivu, karibu ya kawaida mno. Lakini katika kitabu cha Esta, mambo ya kawaida hubeba uzito usio wa kawaida. Hakuna malaika anayetokea. Hakuna nabii anayenena. Hakuna bahari inayopasuka. Hakuna moto unaoshuka kutoka mbinguni. Mfalme anakosa tu usingizi.
Kisha anaagiza vitabu vya kumbukumbu za ufalme visomwe mbele yake. Wasomaji “wanatokea” kukutana na habari ya uaminifu wa Mordekai. Mfalme “anatokea” kugundua kwamba Mordekai hakuwahi kutuzwa. Hamani “anatokea” kufika wakati huo huo, akiwa amekuja kuomba Mordekai auawe.
Na kabla Hamani hajafungua kinywa chake kuzungumzia kifo, mfalme anamwulizia namna ya kumheshimu mtu ambaye mfalme amependezwa naye.
Sura hii inafunua jinsi uaminifu uliosahaulika unavyoweza kugeuzwa kuwa mlango wa unaofungulia ushindi wa wazi—kwa sababu Mungu anayetenda kwa siri, ana uwezo wa kuamsha kumbukumbu katika saa ileile ambayo uovu unajihakikishia ushindi. [1]
Kitabu cha Esta kinatufundisha kusoma historia kwa macho yaliyofundishwa. Mungu hatajwi kwa jina, lakini hayupo mbali. Jina lake limejificha, lakini alama za vidole vyake ziko kila mahali. Majaliwa ya Mungu hayaji kila wakati kwa ngurumo. Wakati mwingine huja kwa kukosa usingizi, makaratasi ya kumbukumbu, muda uliopangwa vizuri, kutoelewana, na mabadiliko ya ghafla yanayoweza kushusha kiburi hadi chini. [2]
Hamani anafikiri asubuhi ni mali ya hasira yake. Lakini kabla ya alfajiri, majaliwa tayari yamegeuza uelekeo wa mambo.
Mti wa kunyongolea uko tayari.
Lakini farasi naye yuko tayari.
2.0 Muktadha wa Kihistoria na Kifasihi: Mahali pa Kugeukia kwa Simulizi
Esta 6 inasimama katikati ya mageuzi makubwa ya kitabu. Nusu ya kwanza ya simulizi inamalizikia: Vashti anaondolewa, Esta anachukuliwa ikulu, Hamani anainuliwa, Mordekai anatishiwa, Wayahudi wanahukumiwa, na mti wa kunyongolea unachongwa. Baada ya sura ya 6, mwendo unaanza kuchanganyia: Hamani anafichuliwa, Mordekai anainuliwa, amri ya pili inatolewa, Wayahudi wanaokoka, na maombolezo yanakuwa sikukuu.
Kwa hiyo, sura hii haitusimulii tukio la pembeni. Ni la katikati, la kibawaba, na la kigurudumu linalogeuza mwenendo wa simulizi. Hata hivyo, kitabu kizima ni hadithi ya mageuzi: wenye kiburi wanashushwa, waliopuuzwa wanainuliwa, mtego unamnasa aliyeutengeneza, kilichojificha kinaonekana, na kilichosahaulika kinakumbukwa. [3]
Karamu mbili za Esta pamoja na mfalme na Hamani zinauzunguka usiku huu wa majaliwa. Katika sura ya 5, Esta anawaalika kwenye karamu ya kwanza na kuchelewesha ombi lake. Katika sura ya 7, kwenye karamu ya pili, anamfichua Hamani. Katikati ya meza hizo mbili ndipo unakuja usiku huu wa majaliwa, ambapo uaminifu uliosahaulika wa Mordekai unakumbukwa, na kiburi cha Hamani kinaanza kuporomoka.
Sura hii pia hukusanya nyuzi zilizofumwa mapema. Katika Esta 2, Mordekai alifunua njama dhidi ya mfalme. Tukio hilo liliandikwa, lakini Mordekai hakupata thawabu. Kumbukumbu hiyo iliyosahaulika sasa inarudi kwa wakati sahihi kabisa, wakati Hamani anamtaka afe. Katika Esta 3, Hamani aliinuliwa na Mordekai akakataa kumsujudia. Sasa Hamani atalazimika kumheshimu Mordekai hadharani. Katika Esta 5, Hamani alijenga mti wa kunyongea. Sasa, kabla hajautumia, atalazimika kumtembeza Mordekai mjini.
Mageuzi ni kama ya Yusufu kule Misri, ambaye huduma yake ilisahaulika gerezani mpaka usiku wenye misukosuko wa Farao ulipomrudisha kwenye kumbukumbu (Mwa. 40:23; 41:1–14). Ni kama Danieli uhamishoni, ambapo mahakama za falme za kigeni zinakuwa jukwaa ambalo Mungu huzishusha nguvu zenye kiburi na kuwathibitisha mashahidi waaminifu (Dan. 2:1–23; 6:18–23). Ni kama Kutoka, ambapo ukombozi wa Israeli unakuja katika usiku uliokesha mbele za Bwana (Kut. 12:42). Zaidi ya yote, mageuzi yanaelekeza mbele kwenye habari ya kwamba jiwe lililokataliwa linakuwa jiwe kuu la pembeni, Masihi aliyesulubiwa anafufuliwa, na msalaba wa aibu unakuwa kiti cha enzi cha hekima ya Mungu iokoayo (Zab. 118:22–23; Mdo. 2:23–24; 1 Kor. 1:18–25; Flp. 2:5–11).
Esta 6 pia imejaa kejeli ya kifasihi. Hamani anaposikia swali la mfalme, moyo wake unamshawish kuamini mara moja kwamba swali hilo haliwezi kuwa juu ya mtu mwingine isipokuwa yeye. Mawazo yake yanafunua njaa yake: mavazi ya kifalme, farasi wa mfalme, taji, msafara, na tangazo la hadharani. Anabuni heshima anayoitamani yeye mwenyewe, kisha anaamriwa kumpa heshima hiyo mtu anayemchukia.
Sura hii inachekesha, lakini si kwa kufurahisha tu. Ucheshi wake unatumikia haki. Inatufundisha kwamba mamlaka yenye kiburi inaweza kuonekana ya kutisha, lakini mbele ya hekima ya Mungu ni ya kipuuzi pia. Kiburi cha Hamani kinampofusha, na upofu wake unakuwa njia ya kudhalilishwa kwake.
Mungu hatajwi.
Lakini kila mstari katika sura hii unapaza sauti kwa unyenyekevu: hapa kuna alama za vidole vya Mungu.
3.0 Kutembea Ndani ya Andiko
3.1 Mfalme Anapokosa Usingizi (Esta 6:1)
“Usiku ule mfalme hakupata usingizi.”
Huu ni usiku uleule ambao mti wa Hamani umesimama tayari. Ni usiku kabla ya karamu ya pili ya Esta. Ni usiku kabla Hamani hajapanga kuomba kifo cha Mordekai. Muda hapa ni kila kitu.
Katika simulizi nyingine ya Biblia, tungetarajia ndoto kutoka kwa Mungu, neno la kinabii, au malaika kutokea. Lakini Esta anatupa kukosa usingizi. Mtu mwenye nguvu kuliko wote katika dola hana utulivu, na kukosa utulivu kwake kunakuwa mlango wa ukombozi.
Mfalme anaagiza kitabu cha kumbukumbu za mambo makuu kisomwe mbele yake. Labda anatarajia kumbukumbu hizo zimletee usingizi. Lakini chombo cha kumbukumbu za dola kinakuwa chombo cha majaliwa ya Mungu.
Esta imetufundisha kuangalia mambo madogo: nafasi iliyotokea ikulu, kibali machoni pa maafisa, njama iliyosikiwa kwa bahati, thawabu iliyocheleweshwa, karamu iliyoahirishwa, usiku usio na usingizi. Mungu aliyejificha mara nyingi hufanya kazi kupitia mambo ya kawaida sana kiasi kwamba wenye kiburi hawawezi kuyatambua. [4]
Mfalme hakupata usingizi.
Lakini majaliwa yako macho kabisa.
Na nyuma ya mfalme aliyekosa usingizi yuko Mungu ambaye “hatasinzia wala hatalala” (Zab. 121:4). Macho ya dola yanakuwa mazito, lakini Mlinzi wa Israeli anakaa macho.
3.2 Kumbukumbu Iliyosahaulika Inaposema (Esta 6:2–3)
Kumbukumbu za ufalme zinasomwa, na taarifa inapatikana jinsi Mordekai alivyowafichua Bigthana na Tereshi, matowashi wawili wa mfalme waliopanga njama dhidi ya Ahasuero. Mfalme anauliza, “Mordekai amepewa heshima gani au cheo gani kwa jambo hili?”
Jibu linashangaza: “Hakuna alilofanyiwa.”
Hapa ndipo uchungu wa kutotambuliwa kwa wakati wake unaonekana. Mordekai aliokoa maisha ya mfalme, lakini dola ilimsahau. Uaminifu wake uliandikwa, lakini haukutuzwa. Huduma yake ilitoweka kwenye makabrasha ya ufalme.
Lakini kile wanadamu wanachosahau, majaliwa ya Mungu yanaweza kukirudisha. Kuchelewa kuliumiza, lakini kuchelewa huko pia kuliweka thawabu mahali pake, kwa wakati uleule Mordekai alipohitaji kuokolewa. Kama Mordekai angeheshimiwa mapema, kumbukumbu hiyo huenda isingemwokoa sasa. Tendo lililosahaulika linakuwa na nguvu kwa sababu lilibaki halijamalizwa.
Hii haifanyi kupuuzwa kuwa jambo jema. Haifanyi kusubiri kuwa rahisi. Haimaanishi kila kuchelewa kwa uchungu ni siri tamu. Lakini inatufundisha kwamba uaminifu uliofichwa haupotei bure. Utii mwingine hupandwa kama mbegu gizani. Unaonekana kama umezikwa, lakini kwa wakati wa Mungu huota.
Yusufu aliijua njia hii. Alitafsiri ndoto ya mnyweshaji na kuomba akumbukwe, lakini mnyweshaji alimsahau mpaka ndoto ya Farao ilipofungua mlango wa gereza (Mwa. 40:14, 23; 41:9–14). Baadaye Yusufu aliweza kutazama nyuma na kusema, “Mungu aliyakusudia kuwa mema” (Mwa. 50:20). Esta 6 inasimama ndani ya mto huohuo wa tumaini la kibiblia: kinachoonekana kimesahaulika bado kinaweza kuwa mikononi mwa Mungu.
Hapa ndipo swali la mfalme linapopindua majira. Wakati uovu ukitafuta kumvua Mordekai utu na kumvika aibu, mamlaka inatafuta kumvika heshima iliyocheleweshwa.
Wakati Hamani akisubiri nje, ule mti wa kunyongea unaanza kutetemeka chini ya uzito wa hukumu ya kimya.
3.3 Hamani Anapowahi Mapema Akiwa na Kifo Moyoni (Esta 6:4–5)
Wakati huohuo, mfalme anauliza, “Ni nani aliye uani?” Hamani alikuwa ameingia tu katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme ili aseme naye habari ya kumnyonga Mordekai juu ya mti aliomwandalia.
Muda hapa ni wa ajabu kiasi cha kuonekana kama mzaha mtakatifu. Esta anataka tuhisi kejeli yake. Hamani anakuja mapema, akiwa na shauku ya kugeuza hasira yake ya ndani kuwa mauaji ya hadharani. Lakini anafika mara tu baada ya mfalme kukumbuka uaminifu wa Mordekai.
Watumishi wanatangaza kwamba Hamani amesimama uani. Mfalme anasema, “Aingie.”
Hamani anaingia akiwa amebeba kifo, lakini mfalme hajui hilo. Mfalme amebeba swali la heshima, lakini Hamani hajui hilo. Ajenda mbili zinaingia chumba kimoja: ajenda ya Hamani ya mauaji na ajenda ya majaliwa ya Mungu ya kugeuza mambo.
Uovu hauko na udhibiti mkubwa kama unavyodhani. Hamani amepanga mti, amechagua asubuhi, amejipa moyo, na ameingia uani. Lakini tayari amechelewa mbele ya majaliwa yaliyoanza kabla hajafika.
Waovu wanaweza kufika mapema.
Lakini Mungu hachelewi kamwe.
3.4 Kiburi Kinapojibu Tamaa Yake Yenyewe (Esta 6:6–9)
Mfalme anamwuliza Hamani, “Afanyiwe nini mtu ambaye mfalme amependezwa kumheshimu?”
Mara moja Hamani anawaza, “Ni nani ambaye mfalme angependa kumheshimu zaidi yangu?” Hii ndiyo sauti ya ndani ya kiburi. Hamani hawezi kufikiria ulimwengu ambao heshima haimhusu yeye. Kiburi chake kimevimba kiasi ja kumjaa kichwan hata asielewa uzito wa swali linaloulizwa.
Kwa hiyo, anabuni itifaki ya kifahari inayolenga kuiba utukufu wa mfalme. Mavazi ya kifalme yaletwe, ambayo mfalme ameyavaa. Farasi aletwe, ambaye mfalme amempanda, na taji ya kifalme iwe juu ya kichwa chake. Mmoja wa wakuu wa mfalme amvishe mtu huyo na kumtembeza katika uwanja wa mji, akitangaza, “Hivyo ndivyo atakavyofanyiwa mtu ambaye mfalme amependezwa kumheshimu.”
Jibu la Hamani linafunua ujazo wa moyo wake. Hataki tu mali au cheo. Anataka kutambuliwa hadharani. Anataka kuonekana kama mfalme. Anataka mji wote usikie ukubwa wake ukitangazwa. Anataka heshima ionyeshwe, ionekane, na ipaziwe sauti.
Hili ndilo jaribu la tangu zamani la kiburi cha mwanadamu: kunyakua utukufu badala ya kuupokea kama zawadi. Edeni, mwanadamu alinyosha mkono kutafuta hadhi ya kuwa kama Mungu (Mwa. 3:5–6). Babeli, wanadamu walijenga kwenda juu ili kujifanyia jina (Mwa. 11:4). Ndani ya Hamani, kasumba ileile imevaa mavazi ya Uajemi.
Hekima ya Biblia iko wazi: “Kiburi hutangulia uangamivu” (Mit. 16:18), na “kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu” (Mit. 18:12). Baadaye Yesu atafundisha mantiki hiyohiyo ya ufalme: “Ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” (Mt. 23:12). Huu ndio upofu wa Hamani: hawezi kuifahamu hekima hii mpaka pale anguko lake linapofanywa somo la vizazi.
Kejeli hii inakata hadi mifupa.
Hamani anaandika mpango wa kumtukuza Mordekai.
Akili ya kiburi chake inakuwa mtego wa fedheha yake.
3.5 Mwenye Kiburi Anapoongoza Farasi (Esta 6:10–11)
Kisha mfalme anatamka maneno yanayogeuza dunia ya Hamani: “Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, ukamfanyie vivyo Mordekai Myahudi, aketiye langoni pa mfalme. Usiache neno lo lote katika yote uliyosema.”
Mordekai Myahudi.
Utambulisho ambao Hamani anauchukia sasa unatamkwa na mfalme katika muktadha wa heshima. Mtu ambaye Hamani anataka kumnyonga lazima avikwe mavazi ya kifalme. Mtu ambaye hakusujudu lazima atembezwe mjini. Mtu ambaye Hamani alitaka kumwaibisha lazima ainuliwe hadharani.
Na Hamani lazima aongoze farasi.
Huu ndio uzuri wa kichekesho katika kitabu cha Esta. Mawazo ya Hamani mwenyewe yanageuka kuwa adhabu yake. Sasa analazimika kuongoza sherehe ya kumtukuza mtu yuleyule aliyemtesa nafsi yake kwa kumkatalia heshima. Lazima awe mtangazaji wa kuinuliwa kwa Mordekai.Kinywa chake sasa kinalazimika kutangaza utukufu wa mtu yuleyule ambaye jina lake alitafuta kulifuta kabisa chini ya jua.
Wakati huu unatukumbusha tena Yusufu. Yusufu anavikwa mavazi ya kifalme, anapewa heshima hadharani, na anainuliwa katika dola ya kigeni ili kuhifadhi uhai (Mwa. 41:42–45; 45:5–7). Heshima ya Mordekai bado si kuinuliwa kwake kwa mwisho, lakini ni ishara ya kwanza kwamba simulizi imegeuka. Aliyewekewa alama ya kifo anavikwa heshima. Aliyepanga kifo anakuwa mtumishi wa mabadiliko. [5]
Lakini Mordekai hashiki madaraka kwa pupa. Hajisifu. Hasemi neno. Anapokea heshima iliyokuja kwa muda wa ajabu wa majaliwa.
Mageuzi yameanza, lakini hayajakamilika. Amri ya kifo bado ipo. Wayahudi bado wako hatarini. Esta bado hajatoa ombi lake. Lakini mwelekeo wa simulizi umebadilika.
Mwanga wa kwanza wa ukombozi umeingia gizani.
3.6 Hamani Anaporudi Akiwa Amefunikwa na Maombolezo (Esta 6:12–14)
Baada ya msafara, Mordekai anarudi langoni pa mfalme. Hii ni sehemu ya kushangaza. Heshima haimfanyi kuwa na tamaa ya kujitangaza. Anarudi kwenye nafasi yake. Anabaki thabiti.
Lakini Hamani anakimbilia nyumbani akiwa katika maombolezo, amefunika kichwa chake. Mtu aliyetaka Mordekai adhalilishwe hadharani sasa yeye mwenyewe anabeba aibu. Hapo awali, Mordekai alivaa magunia katika huzuni ya hadharani (Est. 4:1). Sasa Hamani anavaa alama za kudhalilishwa. Mabadiliko yanaanza kuonekana hata katika mavazi na mkao.
Hamani anawaambia Zeresh na rafiki zake yote yaliyotokea. Ushauri wao unabadilika ghafla. Wale wale waliomtia moyo kujenga mti sasa wanatafsiri kudhalilishwa kwake kama mwanzo wa kuanguka kwake. Wanasema, “Ikiwa Mordekai, ambaye umeanza kuanguka mbele yake, ni wa uzao wa Wayahudi, hutamweza; bali hakika utaanguka mbele yake.”
Hii ni mojawapo ya kauli nzito zaidi kitheolojia katika sura hii. Haitoki kwa nabii, wala kwa Esta, wala kwa Mordekai, bali kwa nyumba ya Hamani mwenyewe. Wanatambua kwamba kuna jambo kubwa kuliko tukio hili linaloendelea. Kuanguka kwa Hamani mbele ya Mordekai si aibu ya kawaida; ni ishara ya kuporomoka kusikozuilika. [6]
Neno “kuanguka” linasikika katika sura hii kama kengele. Hamani ameanza kuanguka, na hakika ataanguka. Mtu aliyedai wengine wamsujudie atashushwa chini.
Kabla hawajamaliza kusema, matowashi wa mfalme wanafika na kumharakisha Hamani kwenda kwenye karamu ya pili ya Esta. Hana muda wa kupumzika vya kutosha, hana muda wa kufikiri upya, hana muda wa kubadili njia. Anachukuliwa kutoka kudhalilishwa moja kwa moja kwenda kufichuliwa.
Usiku uliokosa usingizi umefanya kazi yake.
Sasa meza imeandaliwa.
4.0 Tafakari ya Kitheolojia
4.1 Majaliwa Yaliyofichwa Hufanya Kazi Kupitia Njia za Kawaida
Esta 6 ni mojawapo ya picha kuu za Maandiko kuhusu majaliwa yasiyo na maonyesho makubwa. Mfalme anakosa usingizi. Kitabu kinasomwa. Kumbukumbu inapatikana. Swali linaulizwa. Hamani anafika kwa wakati mbaya ulio sahihi. Mordekai anaheshimiwa.
Hakuna tukio moja kati ya haya linaloonekana kuwa muujiza peke yake. Lakini kwa pamoja, yanakuwa muujiza wa muda uliopangwa. Esta inatufundisha kuamini kwamba ukimya wa Mungu sio utupu; mamlaka yake yaliyofichama yanatenda kazi kupitia matukio ya kawaida kabisa, bila kupoteza hata chembe ya uungu wake. [7]
Somo hili ni muhimu kwa imani. Mara nyingi tunamtafuta Mungu katika mambo makubwa tu. Esta inatufundisha kuona majaliwa katika mipangilio tulivu: kumbukumbu inayoamshwa kwa wakati wake, mazungumzo yanayotokea kabla ya madhara, kuchelewa kunakogeuka kuwa ukombozi, mlango uliofungwa unaotulinda, mlango uliofunguka bila kutarajia.
Mungu anaweza kugeuza upepo.
Anaweza pia kumfanya mfalme akose usingizi.
4.2 Uaminifu Uliosahaulika Haupotei Bure
Uaminifu wa Mordekai katika sura ya pili haupati thawabu ya haraka. Lakini sura ya sita inaonyesha kwamba kile kinachosahaulika na dola, kinalindwa salama katika utendaji uliojificha wa Mungu.
Waumini wengi wanaishi na utii uliofichika: maombi ambayo hakuna aliyeyasikia, sadaka ambazo hakuna aliyeshukuru, huduma ambayo hakuna aliyeitambua, na uadilifu ambao hakuna aliyeulipa. Esta 6 haitoi ahadi ya juu juu kwamba kila tendo la uaminifu litapata heshima ya hadharani mara moja. Lakini inasimama kama ushuhuda thabiti kwamba uaminifu kamwe haupotei kwenye ombwe mbele za Mungu.
Paulo analipa kanisa neno hilohilo la kichungaji akisisitiza kuwa taabu yenu si bure katika Bwana (1 Kor 15:58). Mwandishi wa Waebrania naye anakumbusha kwamba Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu na pendo mlilolionyesha kwa jina lake (Ebr 6:10). Hata Yesu mwenyewe anathibitisha kwamba Baba huona yatendwayo sirini (Mt 6:4, 6, 18).
Ufalme wa Mungu unatunza kumbukumbu tofauti kabisa na mifumo ya wanadamu. Mbinguni hakuna maktaba inayofunikwa na mavumbi.
4.3 Kiburi Ni Kipofu Kabla Hakijaanguka
Kuanguka kwa Hamani kunaanza pale anaposhindwa kabisa kufikiria kwamba heshima inaweza kuwa ya mtu mwingine. Kiburi hupunguza ulimwengu wa mtu mpaka nafsi yake inakuwa mhimili pekee unaozungusha kila wazo.
Upofu huu unamfanya awe rahisi kunaswa kwenye mtego wa kejeli. Anabuni kwa ustadi heshima ya Mordekai kwa sababu anadhani anajenga utukufu wake mwenyewe; anaongoza farasi barabarani kwa sababu akili yake imegoma kukubali kuwa kuna mwingine anayestahili kutuzwa.
Ushuhuda wa Biblia unaonya mara kwa mara kwamba kiburi huanguka chini ya uzito wake chenyewe. Farao anaufanya moyo wake kuwa mgumu na kuishia kumpoteza mzaliwa wake wa kwanza (Kut 7–12). Nebukadneza anajisifu juu ya ukuu wa Babeli na kushushwa hadhi hadi kiwango cha mnyama (Dan 4:28–33). Herode naye anapokea sifa kana kwamba ni mungu, kisha anaanguka ghafla chini ya hukumu (Mdo 12:21–23).
Kitabu cha Esta kinaongeza ukweli mzito zaidi: mara nyingi kiburi hushiriki kikamilifu katika kujidhalilisha chenyewe. Maneno, mipango, na tamaa za wenye kiburi hugeuka kuwa zana halisi zinazowafichua na kuwaangusha.
4.4 Kugeuzwa kwa Mambo Ndilo Umbo la Tumaini la Kibiblia
Esta 6 si ukombozi wa mwisho, lakini ni mahali ambapo mwelekeo wa mambo unabadilika kabisa. Sura hii inatanguliza mpangilio utakaodhihirika kikamilifu baadaye: Hamani anaanguka, Mordekai anainuka; maombolezo yanakuwa furaha; na amri ya kifo inajibiwa na amri ya uzima.
Kugeuka kwa mambo namna hii kunashuhudiwa katika Maandiko yote. Mungu humchagua mdogo badala ya mkubwa, tasa anakuwa mama, mtumwa anakuwa mtawala, kijana mchungaji anakuwa mfalme, wahamishwa wanakuwa mashahidi, na jiwe lililokataliwa na waashi linakuwa jiwe kuu la pembeni (Mwa 21:1–7; 25:23; 41:41–45; 1 Sam 16:11–13; Zab 118:22–23).
Katika wimbo wa Mariamu, Mungu huwashusha wenye nguvu kutoka kwenye viti vyao vya enzi na kuwainua wanyenyekevu (Lk 1:52). Katika Yesu, mpangilio huu unafika kileleni mwake. Msalaba ulionekana kama ushindi wa dola, mashtaka, na kifo. Lakini ufufuo ulifunua kwamba kile chombo cha aibu kilikuwa madhabahu ya ushindi wa Mungu. Aliyekataliwa aliinuliwa. Aliyehukumiwa akawa Bwana. Mfalme aliyesulubiwa akawa Mwokozi mwaminifu.
Katika kiini cha mapambano haya, Esta 6 inabeba mwangwi wa injili: usiku unaweza kuwa mweusi, na mti wa kunyonga unaweza kuwa umesimama, lakini Mungu ana uwezo wa kubadili uelekeo wa historia kabla ya mapambazuko.
4.5 Majaliwa Hayafuti Ujasiri wa Mwanadamu
Esta 6 inahusu majaliwa, lakini si majaliwa yanayohalalisha kukaa bila kufanya kitu. Usiku ule mfalme alipokosa usingizi haufuti ujasiri wa Esta, ushuhuda wa Mordekai, wala kufunga kwa jamii nzima. Kazi ya Mungu iliyofichika haifanyi utii wa mwanadamu kuwa jambo lisilohitajika; badala yake, inaufanya utii huo uwe na maana ya dhati.
Mordekai alikuwa ametenda kwa uaminifu katika sura ya pili, na Esta akasimama kwa ujasiri katika sura ya nne na ya tano. Wayahudi nao walikuwa wameingia katika maombolezo na saumu katika sura ya nne. Usiku ule uliokosa usingizi hauchukui nafasi ya matendo haya ya uaminifu, bali unayakusanya na kuyaunganisha ndani ya mpango mkuu wa Mungu.
Ukweli huu unabeba uzito mkubwa kwa ajili ya uanafunzi, uongozi wa kanisa, na utume wetu. Kuamini majaliwa si kukunja mikono wakati uovu ukiwa bize kuchonga miti ya kunyongea; ni kutenda kwa uadilifu chini ya uhakika thabiti kwamba Mungu tayari anasogeza mambo mbali zaidi ya yale yanayonekana kwa macho ya nyama.
5.0 Matumizi ya Maisha: Uaminifu Katika Usiku wa Kusubiri
1. Kusahaulika Kusitafsiriwe Kama Kupotea Bure. Uaminifu wa Mordekai ulikaa gizani bila kutuzwa kwa miaka mingi, hadi pale majira sahihi ya kimungu yalipowadia. Unapoona kutambuliwa kwako kunachelewa, endelea kusimama katika nafasi yako kwa uaminifu usiotikisika. Thawabu ya haraka si uthibitisho wa rehema ya kina kila wakati; mara nyingi, Mungu anachelewesha heshima ili kuiweka mahali ambapo itatumikia kusudi kubwa zaidi kuliko unavyowaza.
2. Jihadhari na Nafsi Inayojizungusha Yenyewe. Ugonjwa mkuu wa Hamani ulikuwa upofu wa kutoweza kuona mwingine yeyote isipokuwa yeye mwenyewe kama mtu pekee anayestahili kutukuzwa. Ni vyema kujihoji kila mara: ni wapi ambapo kiburi kimepunguza upeo wako na kuufanya ulimwengu wako kuwa mdogo kiasi cha kuona mambo yakikuhusu wewe pekee?
3. Ruhusu Heshima Ikunyenyekeshe. Baada ya kuvishwa vazi la kifalme na kupitishwa barabarani kwa shangwe kuu hadharani, Mordekai hakubadilika—alirejea kimya kimya kwenye lango la mfalme kuendelea na majukumu yake. Uhakika wa kutambuliwa na Mungu hauhitaji majivuno; kibali cha kweli kinapaswa kukuacha ukiwa magoti chini katika unyenyekevu.
4. Mtazame Mungu Katika Vitu vya Kawaida. Usiwaze kuwa uwepo wa Mungu unakuja tu kwa ngurumo au miujiza inayotikisa ardhi. Kukosa usingizi kwa mfalme, makaratasi ya kumbukumbu za zamani, mazungumzo ya ghafla asubuhi, na usahihi wa sekunde chache—vyote hivi ni vyombo safi vya neema ambavyo Mungu anavitumia kusogeza historia.
5. Usiogope Wakati Uovu Unapoonekana Kukamilisha Maandalizi Yake. Hamani alikuwa na mti mrefu tayari kule nje, na alikuwa na ratiba thabiti ya asubuhi hiyo kichwani mwake. Lakini kabla hajatenda, Mungu tayari alikuwa na mfalme aliyepoteza usingizi na kumbukumbu ya uaminifu iliyoamshwa kwa wakati. Pale adui anapofikiri asubuhi ni mali ya hasira yake, Mungu anakuwa ameshabadili uelekeo wa mambo tangu usiku.
6. Ishi kwa Uaminifu Katika Mazingira ya Uhamisho. Mordekai alitumika kwa uadilifu mkubwa ndani ya ikulu ya kigeni ya Shushani, bila kusalimisha hata chembe ya utambulisho wake wa kiimani. Vivyo hivyo, wanafunzi wa Yesu leo wameitwa kushuhudia kwa hekima na msimamo thabiti katika maeneo yao ya kazi, kwenye taasisi, mitaani, miongoni mwa majirani, na katika maisha yote ya umma.
7. Tambua Kwamba Mapinduzi ya Kimungu Huanza Kimya Kimya. Kabla ya ukombozi mkuu kushuhudiwa na watu wote hadharani, kazi ya Mungu huanza gizani—akiamsha kumbukumbu zilizofunikwa na mavumbi, akifunua kiburi kilichojificha, na kubadili hatima ya mambo kabla ya mapambazuko kufika.
6.0 Uanafunzi, Uongozi wa Kanisa, na Utume
6.1 Kwa Uanafunzi: Kuwa Mwaminifu Wakati Hakuna Anayeangalia
Esta 6 inawaita wanafunzi wa Yesu kwenye uaminifu uliojificha. Mordekai alifanya jambo lililo sawa katika sura ya 2 bila kujua kama angewahi kuheshimiwa. Huo ndio udongo wa uanafunzi wa kweli: utii bila makofi.
Mwanafunzi humfuata Yesu si kwa sababu kila tendo linaonekana mara moja, bali kwa sababu Baba huona sirini. Kanisa lazima liwafundishe waumini kutumika bila kuhitaji kuonekana kila mara, kuomba bila kufanya maigizo, kuishi kwa uadilifu bila thawabu, na kubaki imara wakati kutambuliwa kunachelewa.
Njia ya Yesu si msafara wa Hamani wa kujionyesha. Ni njia ya msalaba, njia ya uaminifu wa unyenyekevu.
6.2 Kwa Uongozi wa Kanisa: Wakumbukeni Watumishi Waliosahaulika
Kushindwa kwa mfalme kulikuwa kushindwa kwa kumbukumbu. Mordekai aliokoa maisha yake, lakini dola ilimsahau. Esta 6 inawaonya viongozi kwa sauti tulivu: taasisi zinaweza kutunza rekodi ya huduma bila kuwaheshimu wahudumu.
Viongozi wa kanisa lazima wajenge kumbukumbu takatifu. Ni nani ametumika kimya kimya? Ni nani amebeba mizigo bila sifa? Ni nani amelinda jamii, amefundisha watoto, ametembelea wagonjwa, ameomba sirini, amesafisha chumba, amembeba aliyejeruhiwa, au amebaki mwaminifu langoni?
Uongozi unakuwa na sura ya ufalme wa Mungu zaidi pale unapokataa kuwaacha watu waaminifu wapotelee kwenye makabrasha yaliyojaa vumbi.
Wachungaji wema hukumbuka.
Na wanapokumbuka, wanasaidia jamii kuwa nyumba ya shukrani.
6.3 Kwa Utume: Mungu Hufanya Kazi Katikati ya Mchanganyiko wa Maisha ya Umma
Esta ni kitabu cha watu walio uhamishoni. Watu wa Mungu hawako Yerusalemu. Wako Shushani, ndani ya dola yenye utata wa kimaadili. Hata hivyo Mungu hayupo mbali na mahali hapo. Anafanya kazi ikulu, kupitia kumbukumbu, muda, ujasiri, na ushuhuda wa hadharani.
Utume leo mara nyingi hutokea katika maeneo kama hayo: ofisini, shuleni, kwenye siasa, kwenye vyombo vya habari, hospitalini, magerezani, sokoni, mitaani, na ndani ya familia. Kanisa lisidhani kwamba Mungu hufanya kazi ndani ya majengo ya misheni pekee. Esta inatufundisha kutambua mkono wa Mungu uliojificha katika maisha ya umma na kujiunga na kazi yake kwa hekima, ujasiri, na unyenyekevu.
Utume si kuhubiri kutoka mimbarani tu. Wakati mwingine ni uwepo wa uaminifu langoni. Wakati mwingine ni hotuba ya ujasiri mezani. Wakati mwingine ni kukataa kusujudu mbele ya sanamu za mamlaka. Wakati mwingine ni kutunza tumaini mpaka usiku upishe mapambazuko.
6.4 Kwa Jamii Zilizoko Chini ya Shinikizo: Tumaini Lisilo na Ujinga
Esta 6 haikanushi ukubwa wa hatari iliyopo. Mti wa kunyongolea ni halisi, amri ya maangamizi ni halisi, na chuki ya Hamani ni ukweli usiopingika. Tumaini la kibiblia si kujifanya kwamba usiku hauna madhara au hauna nguvu; bali ni uhakika thabiti kwamba usiku huo haubebi neno la mwisho la hatima yetu.
Jamii zilizoko chini ya shinikizo na majaribu mazito zinahitaji tumaini la aina hii—matumaini yasiyo na wepesi wa juu juu, yasiyokataa ukweli wa mambo, na yasiyotokana na hofu iliyovishwa lugha ya kidini. Badala yake, ni ujasiri wa utulivu wa ndani unaoamini kwamba Mungu ana uwezo wa kutenda kazi kwa ustadi mkubwa, hata katika majira ambayo uwepo wake hauonekani wazi juu ya uso wa matukio.
Kanisa lazima liwe jamii ya watu wanaoweza kuutazama mti wa kunyongea ukiwa umesimama, na bado wakasimama imara na kutangaza kwa ujasiri: Mungu hajamaliza kazi yake.
7.0 Maswali ya Kutafakari
Ni tendo gani la uaminifu katika maisha yako linaonekana limesahaulika, halijalipwa, au limefichwa?
Ni wapi unahitaji kuamini muda wa Mungu badala ya kudai kutambuliwa mara moja?
Mawazo ya Hamani yaliyojizunguka yenyewe yanakuonyaje kuhusu kiburi ndani ya moyo wako?
Je, umewahi kuona Mungu akitumia jambo la kawaida kubadilisha mwelekeo wa hali fulani?
Ingeonekanaje kwako kurudi kwa uaminifu kwenye “lango” lako baada ya kupokea heshima?
Ni nani katika kanisa lako au jamii yako anayehitaji kukumbukwa, kushukuriwa, na kutiwa nguvu?
Ni wapi Mungu anaweza kuwa tayari ameanza kugeuza mambo ambayo bado huwezi kuyaona kikamilifu?
8.0 Ombi la Mwitikio
Ee Mungu uliyejificha katika usiku usio na usingizi,
Wewe unakumbuka yale ambayo falme husahau.
Unaona tendo la uaminifu lililozikwa katika kumbukumbu,
utii wa kimya ulioachwa bila thawabu,
mtumishi ambaye bado ameketi langoni.
Wakati mti wa kunyongolea umesimama tayari,
ilinde mioyo yetu isikate tamaa.
Wakati uovu unawahi mapema ukiwa na kifo kinywani,
tukumbushe kwamba rehema yako tayari imetutangulia kabla ya asubuhi.
Tuokoe na kiburi cha Hamani,
na upofu unaodhani kila heshima ni yetu,
na njaa ya kuonekana, kusifiwa, kuinuliwa, na kutangazwa.
Tufundishe unyenyekevu wa Mordekai,
kupokea heshima bila kuinyakua,
na kurudi kwa uaminifu kwenye kazi iliyo mbele yetu.
Amsha kumbukumbu mahali ambapo kweli imezikwa.
Fungua kumbukumbu zinazohitaji kusema.
Geuza mipango ya wenye kiburi iwe njia ya kufichuliwa kwao wenyewe.
Acha farasi wa mabadiliko apite mjinimpaka waliochoka wakumbuke kwamba bado unafanya kazi.
Utufanye wanafunzi wa uaminifu uliojificha,
viongozi wanaowakumbuka watumishi waliosahaulika,
na kanisa ambalo utume wake unasonga kwa ujasiri katika uwanja wa maisha ya umma.
Katika jina la Yesu,
aliyekataliwa lakini ukamwinua,
aliyesulubiwa lakini ukamfufua,
Mfalme wetu wa kweli na Mwokozi mwaminifu.
Amina.
9.0 Dirisha la Kinachofuata
Esta 6 inaishia kwa Hamani kuharakishwa kwenda kwenye karamu ya malkia. Hana muda wa kupona baada ya kudhalilishwa. Mtu aliyejenga mti kwa ajili ya Mordekai ametoka tu kumtembeza Mordekai mjini kwa heshima. Nyumba yake mwenyewe imemwonya kwamba ameanza kuanguka.
Sasa meza imeandaliwa kwa ajili ya kufichuliwa.
Katika Esta 7, karamu itageuka kuwa mahakama. Hatimaye Esta atafunua watu wake na kumtaja adui. Mfalme atakasirika. Hamani ataomba rehema. Mti alioujenga kwa ajili ya Mordekai utakuwa mahali pa hukumu yake mwenyewe.
Usiku uliokosa usingizi umegeuza simulizi.
Sasa ukweli uliojificha utaingia nuruni.
10.0 Bibliografia
[1] Levenson, Jon D. Esther: A Commentary. Old Testament Library. Louisville: Westminster John Knox, 1997.
[2] BibleProject. “The Book of Esther.” Old Testament Overview Guide.
[3] Fox, Michael V. Character and Ideology in the Book of Esther. 2nd ed. Grand Rapids: Eerdmans, 2001.
[4] Berlin, Adele. Esther. JPS Bible Commentary. Philadelphia: Jewish Publication Society, 2001.
[5] Clines, David J. A. Ezra, Nehemiah, Esther. New Century Bible Commentary. Grand Rapids: Eerdmans, 1984.
[6] Moore, Carey A. Esther. Anchor Bible 7B. Garden City, NY: Doubleday, 1971.
[7] Wright, N. T. The New Testament and the People of God. Minneapolis: Fortress, 1992.




Comments