WALAWI 10– DHAMBI ISIYOSAMEHEKA: KUDHARAU UTAKATIFU WA MUNGU
- Pr Enos Mwakalindile
- Jul 25
- 6 min read
Updated: Jul 31
Kumkaribia Mungu: Tembelea Walawi, Mtazame Yesu
❓ Je, ni nini kinachotokea tunapodharau utakatifu wa Mungu kwa moto wa kujitungia wenyewe?

UTANGULIZI NA MUKTADHA
Katika mlolongo wa sherehe ya kuanzishwa kwa ukuhani, ambapo kila kitu kilikuwa kinaendelea kwa utaratibu na utukufu, tunashtushwa na simulizi la ghafula—kifo cha Nadabu na Abihu, wana wa Haruni. Walikufa mbele za Bwana kwa sababu waliingia na “moto wa kigeni” ambao Mungu hakuwa ameamuru (Walawi 10:1–2).
Sura hii haizungumzii dhambi za dhahiri kama uasherati au uuaji, bali dhambi ya ibada isiyoelekezwa na Mungu—kuleta moto usiotoka madhabahuni pa Mungu, bali kutoka kwenye vichwa vyao wenyewe. Hii ni simulizi ya kutisha kwa wote wanaotaka kumkaribia Mungu bila unyenyekevu na utakatifu.
Katika kitabu kizima cha Walawi, dhambi si tu kuvunja sheria, bali kuvunja ushirika—kuvua viatu vyako mbele ya ardhi takatifu na kuikanyaga kwa kujitafutia njia zako mwenyewe. Moto wa kigeni haukuwa tu usumbufu wa kiibada, bali jaribio la kuanzisha “mbinu mbadala” za kupata neema.
Hii haikuwa tu kosa la kidini. Ilikuwa jaribio la kuanzisha kanuni mpya ya ibaada—bila neno la Bwana.
SOMA KWANZA – WALAWI 10:1–20
Chukua muda kusoma sura nzima kwa utulivu. Zingatia:
Ni nini kilichokosewa na Nadabu na Abihu?
Majibu ya Mungu, ya Musa, na ya Haruni ni yapi?
Ni mafunzo gani yanayojitokeza kuhusu utakatifu na unyenyekevu?
MUUNDO WA MAFUNZO KWA SURA HII
MOTO WA KIGENI – MISTARI 1–2
Kosa la Nadabu na Abihu linaelezwa kama kuwasha "moto wa kigeni" usio kutoka kwenye madhabahu ya Mungu (Walawi 16:12). Sheria za awali (Kutoka 30:7–9) ziliweka wazi kwamba uvumba unapaswa kuchomwa kwa utaratibu uliowekwa na moto maalum uliotoka kwa Mungu mwenyewe. Kwa kulikiuka hili, walidharau uwepo wa Mungu ulio juu ya sanduku la agano (Kutoka 40:34–35) na hivyo kuleta hukumu ya haraka. Wengine wanasema walihudumu wakiwa wamelewa, jambo lililowaondoa katika umakini wa huduma (linganisha na Walawi 10:8–11). Tukio hili linaonyesha kuwa ibada haiwezi kubadilishwa kulingana na matakwa ya binadamu bali lazima izingatie maagizo ya Mungu (Hesabu 3:4; 26:61).
Swali la majadiliano: Je, leo tunatoa “moto wa kigeni” katika huduma zetu kupitia fahari au tamaa binafsi?
HUKUMU NA UTAKATIFU WA MUNGU (MST. 3–7)
Hukumu hii inafunua utakatifu wa Mungu na wito wa kuwa waangalifu. Musa alikumbusha kauli ya Mungu: “Kwa wale wanaonikaribia nitatakaswa, na mbele ya watu wote nitaheshimiwa” (Walawi 10:3). Kauli hii inahusiana na matukio kama pale ambapo watu walikosa heshima na kupata hukumu, kama Miriam alivyopigwa ukoma kwa kumpinga Musa (Hesabu 12:1–10) na Korah na wafuasi wake walipomezwa na ardhi (Hesabu 16:1–35).
Kwa nini dhambi za aina hii haziwezi kufidiwa kwa damu ya sadaka? Kwa sababu zinawakilisha dharau ya moja kwa moja kwa uwepo wa Mungu na maagizo yake, zikibomoa msingi wa agano na kuonyesha uasi wa makusudi dhidi ya utawala wa Mungu. Sadaka za damu ziliwekwa kwa ajili ya dhambi zisizokusudiwa au upungufu wa kibinadamu (Walawi 4:1–3), lakini makosa ya kiburi na ya kukusudia kuasi kama haya yalihesabiwa kama “kukatiliwa shingo kwa kujitakia” (Hesabu 15:30–31) na yalihitaji hukumu ya moja kwa moja ya Mungu badala ya upatanisho wa dhabihu. Utakatifu wa Mungu unahitaji heshima na unyenyekevu wa ndani, si ibada ya juu juu.
Haruni alinyamaza, akionyesha unyenyekevu wa ndani na kukubali hukumu ya Mungu bila pingamizi, sawa na majibu ya Eli kwa Samweli aliposikia neno la hukumu: “Ndiye Bwana; na afanye alionalo kuwa ni jema” (1 Samweli 3:18).
Swali la majadiliano: Tunawezaje kukuza moyo wa unyenyekevu unaonyamaza mbele ya hukumu ya Mungu?
MARUFUKU YA ULEVI (MST. 8–11)
Baada ya hukumu hiyo, Mungu alitoa amri kwa Haruni na wanawe wasinywe divai au kileo wanapoingia hekaluni (Walawi 10:8–11). Sheria hii inaendana na maelekezo ya Kuhani Mkuu katika Kutoka 28:36–38, ambapo taji la Utakatifu kwa Bwana lilipaswa kuvaliwa kila mara wakiwa safi na wenye akili timamu. Ulevi unamaanisha kukosa umakini na heshima katika kazi ya ibada, hali iliyo kinyume na utakatifu unaohitajika kwa makuhani (Hesabu 6:1–3 kuhusu nadhiri ya Mnadhiri).
Israeli, waliokuwa wameteuliwa kuwa taifa la makuhani (Kutoka 19:5–6), walihitajika kuepuka kuendeshwa na tamaa zinazopumbaza na kuishi kwa umakini na heshima kwa Mungu. Hata hivyo walipoacha wito huu walishindwa kutimiza jukumu lao: walitamani nyama na matamanio yao yakaongoza kwenye kuasi (Hesabu 11:4–10), walitengeneza ndama wa dhahabu wakidhani wanamwabudu Mungu (Kutoka 32:1–8), na walipuuzia amri kuu ya kumpenda Bwana Mungu wao kwa moyo wote (Kumbukumbu la Torati 6:4–9). Taifa la makuhani lilipaswa kumtumikia Mungu wao kwa uangalifu na hofu, utii na heshima anayostahili.
Swali la majadiliano: Ni aina gani za “ulevi wa kiroho” zinazoweza kuharibu huduma zetu leo?
MIGONGANO KUHUSU SADAKA (MST. 12–20)
Musa alikasirika kwa sababu sadaka ya dhambi haikuliwa kama ilivyotakiwa (Walawi 6:19–23). Haruni, akiwa amejaa huzuni kwa tukio la kufa kwa wanawe, alieleza kuwa hali ya moyo wao haikuwa tayari kushiriki chakula kitakatifu cha madhabahuni. Kwa mujibu wa sheria, makuhani walipaswa kula sadaka hizi kwa furaha na shukrani kama ishara ya ushirika na Mungu na kubeba hatia ya watu (Kutoka 29:31–33). Kwa huzuni aliyokuwa nayo, Haruni alihisi kula sadaka hiyo kungekuwa kinyume na heshima kwa Mungu.
Musa aliposikia maelezo hayo alikubali, akitambua kwamba Mungu hutazama moyo wa mtu zaidi ya matendo ya nje (linganisha na Hesabu 18:9–11 kuhusu vyakula vya kikuhani). Tukio hili linafunua kwamba rehema ya Mungu inaweza kuonekana hata katikati ya hukumu kali, akipendelea heshima ya moyo na unyenyekevu kuliko utaratibu wa ibada unaotekelezwa bila ushiriki wa kweli wa moyo.
Swali la majadiliano: Je, hasira ya Musa kuhusu kutokula sadaka inaonyesha nini kuhusu changamoto kati ya kusimamia kwa umakini maagizo ya Mungu na kuchukuana na unyonge wa kibinadamu?
SOMO LA KUJIFUNZA: UTUKUFU WA MUNGU USICHEZEWE
Sura hii inatufundisha kwamba si kila ibada inampendeza Mungu. Nia nzuri haitoshi—utii na utakatifu ni msingi.
Mungu ni Mtakatifu na wa kuogopwa. Ukaribu na Mungu ni kama jua—lenye kutoa nuru na uhai kwa anayekaribia kwa heshima, lakini pia lenye uwezo wa kuchoma na kuangamiza ikiwa mtu atakaribia bila ulinzi na kwa njia isiyoamriwa.
Ibaada haiwezi kujitungia njia zake. Nadabu na Abihu walijaribu kuunda njia yao wenyewe ya kumkaribia Mungu. Ni kama mwana anga anayejaribu kusogea karibu na jua bila mavazi ya kujikinga na moto wake. Matokeo yake yalikuwa ya maangamizi, yakitufundisha kuwa ubunifu usioongozwa na ufunuo unaweza kugeuza nuru kuwa giza.
Yesu Kristo ndiye njia iliyoidhinishwa. Fikiria tukio la Nadabu na Abihu waliokufa kwa kuleta moto wa kigeni—ni somo kali kwamba hakuna wokovu kwa njia yoyote ila kwa njia ya Yesu (Yoh. 14:6). Yeye ndiye Kuhani Mkuu (Waebrania 4:14–16; 5:1–10), anayefungua mlango ili tukaribie kwa ujasiri na heshima, bila hofu bali kwa matumaini.
Hekalu jipya katika Kristo. Yesu alitangaza kuwa mwili wake ni hekalu jipya (Yoh. 2:19-21). Maneno haya yalibadili mtazamo: utakatifu wa Mungu haupo tena tu katika jengo, bali unaishi ndani ya waamini. Sisi, tukiitwa hekalu la Roho Mtakatifu (1 Kor. 6:19-20), tunabeba uwepo wake, jambo linaloongeza uzito na heshima ya maisha matakatifu tunayoishi kila siku.
MATUMIZI YA SOMO MAISHANI
Katika kizazi cha ibada za kitaalamu na burudani ya kiroho, je, tunatambua kwamba moto wa Bwana si wa kuchezea?
Sadaka nzuri si ya kuvutia tu, bali ni ile iliyowekwa wakfu kwa Mungu, kwa moyo uliovunjika.
Jiulize:
Je, ibada yangu ni mwitikio wa ufunuo wa neno la Mungu au ni msukumo wa tamaa zangu?
Je, nimechoka na njia ya kweli kiasi cha kutafuta moto mwingine wa kujiburudisha?
Je, nimejifunza kukaa kimya mbele ya hukumu ya Mungu kama Haruni—au huwa najitetea haraka?
ZOEZI LA KIROHO LA KUTAFUTA MOTO HALISI
Kaa kimya kwa dakika 5 leo, ukiwa umenyamaza mbele za Bwana.
Uliza:
“Ee Bwana, je, nimebeba moto gani wa kigeni? Nioneshe. Nirekebishe.”
Soma Waebrania 12:28–29: “Na tumwabudu Mungu kwa ibaada ya kumpendeza, kwa unyenyekevu na hofu. Kwa maana Mungu wetu ni moto ulao.”
BARAKA YA MWISHO
EE MUNGU MTAKATIFU,
Uliyetukuka juu ya wote,
Usiruhusu roho yangu ilete moto wa kigeni mbele zako.
Nitie moto kutoka madhabahuni pako—moto wa toba,
Moto wa upendo, moto wa utii.
Nitekezee, Bwana, si kwa hasira, bali kwa neema.
Na ibaada yangu iwe harufu nzuri mbele zako.
Kwa jina la Kuhani Mkuu wetu, Yesu Kristo.
Amina.
MASWALI ZAIDI YA KUJADILI KATIKA VIKUNDI
Katika maisha ya kiroho ya leo, “moto wa kigeni” unaweza kuwa nini?
Tunawezaje kuhakikisha ibaada zetu zinafanyika kama atakavyo Mungu, si kujitukuza wenyewe?
Unajifunza nini kutokana na ukimya wa Haruni mbele ya hukumu ya Mungu?
Je, kuna ibada katika jamii yetu ambazo tumezoea lakini zina asili ya moto wa kigeni?
MAELEZO YA VYANZO NA MAREJEO
L. Michael Morales, Who Shall Ascend the Mountain of the Lord? Hoja kwamba Walawi 10 ni onyo kwamba njia ya kumkaribia Mungu lazima iwe njia aliyoweka mwenyewe.
John Walton, The Lost World of Torah, mlango wa miundo ya ibaada – Anaweka muktadha wa sheria za Torati kama mwongozo wa hekalu na makao ya Mungu, badala ya kanuni za maadili pekee.
Ellen G. White, Patriarchs and Prophets, Anaelezea kisa cha “Nadab and Abihu” kama onyo la kiroho dhidi ya ibaada ya kujitungia, na umuhimu wa utii mkamilifu mbele za Mungu.
Jacob Milgrom, Leviticus 1–16 (Anchor Yale Bible) – Maelezo ya kina kuhusu kosa la Nadabu na Abihu kama kutumia “moto wa kigeni” usio kutoka madhabahuni.




Comments