Uchambuzi wa Ayubu 24: Maskini Wanapolia na Usiku Unapoficha Uhalifu
- Pr Enos Mwakalindile
- 1 day ago
- 16 min read
Updated: 3 hours ago

Zipo sura ambamo rundo la majivu hugeuka kuwa dirisha. Ayubu 24 inaanza kwa swali moja la moto: kwa nini Mwenyezi haweki nyakati za hukumu? Kisha Ayubu anaondoa macho kwenye mateso yake mwenyewe na kuutazama ulimwengu uliojeruhiwa na dhuluma—mipaka inahamishwa, mifugo inaporwa, wajane wananyonywa, watoto wanachukuliwa, wafanyakazi wana njaa kando ya mavuno wasiyoruhusiwa kulyaa, maskini wananyeshewa huku wakijisitiri kwenye miamba, wanaokufa wanaugua mjini, na wahalifu wanatumia giza kama pazia lao. Maumivu ya Ayubu yanageuka kuwa macho ya kinabii. Haulizi tu, “Kwa nini ninateseka?” Anauliza pia, “Kwa nini Mungu anawaacha wanaodhulumiwa waendelee kusubiri?”
1.0 Utangulizi: Maumivu ya Binafsi Yanapogeuka Kuwa Kilio cha Haki kwa Jamii
Kuna mateso yanayogeuza macho yetu ndani, yakitufungia katika giza la nafsi zetu. Maumivu yanaweza kuudogosha ulimwengu wote, hadi tusione kingine chochote zaidi ya kovu tulilobeba. Lakini, upo utungu mwingine—wa uzazi zaidi, unaotetemesha kwa mafumbo na sauti ya kinabii—ambao badala ya kutupofusha, unafumbua macho yetu kuyatazama majeraha ya ulimwengu.
Ayubu 24 ni ya aina hiyo ya pili.
Katika Ayubu 23, Ayubu alimtafuta Mungu kila upande. Alitaka kukifikia kiti cha enzi cha Mungu, kuwasilisha hoja yake, na kutangazwa kuwa hana hatia. Lakini Mungu alionekana kujificha—mbele, nyuma, kushoto na kulia. Hata hivyo, Ayubu alikiri kwamba Mungu aliijua njia yake, na kwamba baada ya kujaribiwa angefunuliwa ama dhahabu safi isyo na matope ya lawama za kurushiwa.
Sasa katika Ayubu 24, Ayubu analipanua swali.
Haulizi tu, “Kwa nini siwezi kumpata Mungu?” Anauliza, “Kwa nini wanaodhulumiwa hawazioni nyakati za Mungu kutenda haki?” Hapambanani tu na ukimya wa Mungu katika maisha yake binafsi; anapambana na ukimya huo katika uzoefu mpana wa kijamii. Maskini wananyonywa. Wanyonge wanavuliwa. Wenye njaa wanafanya kazi mashambani na njaa zao. Walio uchi wanalala na baridi bila kujifunika. Mji unaugua. Wauaji, wazinzi na wezi hufanya kazi zao chini ya kifuniko cha giza.
Na Mungu anaonekana kutoingilia kati.
Swala hilo ndilo linaloangaza kama linavyochoma moyo katika sura hii.
Ayubu 24 ni mojawapo ya mashairi makali zaidi ya Biblia kuhusu dhuluma ya kijamii. Mwandishi hajifichi nyuma ya hisia nyepesi au lugha ya kupamba ukweli, bali anajipambanua kwa kufichua waziwazi uovu wa kila siku unaowakandamiza wanyonge: unyakuzi wa ardhi, utepetevu wa haki katika mifugo na madeni, unyonyaji wa yatima na wajane, mishahara isiyokidhi mahitaji, vurugu za mijini, na uovu unaofanyika sirini.
Sura hii inasambaratisha mashtaka ya uongo ya Elifazi kutoka Ayubu 22. Elifazi alidai kimakosa kuwa Ayubu aliwanyima wenye njaa mkate, waliochoka maji, na kuwadhulumu wajane na yatima. Sasa Ayubu anathibitisha kuwa anaijua dhuluma kwa undani zaidi. Hazungumzi kama mnyonyaji anayejificha nyuma ya dini, bali kama mhanga mwenye haki—mwenye jicho linalowaona maskini na moyo unaoomboleza pamoja nao.
Swali kuu la Ayubu 24 ni hili:
Kwa nini Mungu anaiacha dhuluma itawale—na ni imani ya namna gani inayothubutu kuvunja ukimya na kukemea uovu?
Sura hii inazungumzia haki inayochelewa, mateso ya maskini, giza linalohifadhi uovu, na kilio kinachomwomba Mungu aweke siku ambayo mambo yaliyopotoka hatimaye yatanyoshwa.
2.0 Muktadha wa Kihistoria na Kifasihi: Nusu ya Pili ya Hotuba ya Nane ya Ayubu
Ayubu 24 ni jibu la Ayubu linaloendelea kwa hotuba ya tatu ya Elifazi. Katika Ayubu 22, Elifazi alimshutumu Ayubu kwa dhambi za kijamii: kuchukua rehani kwa udhalimu, kuwanyima waliochoka maji, kuwazuia wenye njaa mkate, kuwafukuza wajane mikono mitupu, na kuwaangamiza yatima. Ayubu 23 ilijibu kwa kutamani kumfikia Mungu moja kwa moja. Ayubu 24 inajibu kwa kuugeukia ulimwengu wa wanaodhulumiwa.
Mwendo kutoka sura ya 23 kwenda sura ya 24 ni muhimu kuzingatiwa:
Ayubu 23: Ayubu anatamani kufika katika mahakama ya Mungu kwa sababu anahitaji kuthibitishwa binafsi kuwa hana hatia.
Ayubu 24: Ayubu anatamani hukumu ya Mungu kwa sababu ulimwengu unahitaji haki ya wazi kwa wote.
Kwa maana hiyo, malalamiko ya Ayubu hayajikiti kwenye ubinafsi. Mateso yake binafsi yamekuwa sehemu ya maswali mazito zaidi kuhusu haki na maadili. Kama nadharia ya teolojia ya marafiki zake ingekuwa sahihi, uovu ungeadhibiwa waziwazi na wanyonge wangepewa ulinzi. Mbadala wake, Ayubu anaona hali halisi iliyo kinyume: wenye mamlaka wanawadhulumu walio dhaifu, bila Mungu kuingilia kati mara moja kuwawajibisha.
Muundo wa Ayubu 24 unaweza kueleweka kwa kuugawanya katika sehemu kuu nne:
1. Swali la ufunguzi kuhusu hukumu inayochelewa (24:1).
2. Dhuluma za kijamii na kiuchumi dhidi ya wanyonge (24:2–11).
3. Vurugu za mjini na uhalifu wa mafichoni (24:12–17).
4. Sehemu ngumu ya mwisho kuhusu hatima ya waovu (24:18–25).
Sehemu ya mwisho, aya 18–24, ni mojawapo ya sehemu zinazojadiliwa sana katika kitabu cha Ayubu. Katika Maandiko ya Kiebrania cha Kimasoreti, aya hizi zimo ndani ya hotuba ya Ayubu na zinaonekana kueleza kuanguka kwa waovu kwa lugha inayofanana zaidi na teolojia ya marafiki zake. Baadhi ya wafasiri huziona kama maneno ya marafiki ambayo Ayubu anayakariri kwa kejeli, au kama kukiri kwamba wakati mwingine hukumu hufika. Wengine huona aya hizo kama zimehamishwa na kwamba zingefaa zaidi katika hotuba ya tatu ya Sofari ambayo haipo.
Katika uchambuzi wa sura hii, tunapaswa kuheshimu mahali zilipo katika muundo wa mwisho wa Biblia huku tukitambua mvutano uliopo. Sura yenyewe inatulazimisha kupambana na ugumu uleule ambao Ayubu anaendelea kuufunua: wakati mwingine waovu hustawi; wakati mwingine huanguka; lakini majira ya Mungu kuingilia kati hubaki yamefichika.
Kwa maana hiyo, Ayubu 24 si mjadala mtulivu wa darasani. Isipokuwa, sura hii inasimama
kama hati rasmi ya mashtaka ya kisheria, maombolezo yenye uzito wa kinabii, na kilio cha nguvu kinachopaa kutoka upande wa chini walionyimwa haki katika historia.
3.0 Kutembea Ndani ya Andiko: Ulimwengu Anaouona Ayubu Kutoka Kwenye Majivu
3.1 “Kwa Nini Mwenyezi Haweki Nyakati?”: Swali la Haki Inayochelewa (24:1)
Ayubu anaanza kwa swali:
“Kwa nini Mwenyezi haweki nyakati za hukumu, na kwa nini wale wanaomjua hawazioni siku zake?” (Ayubu 24:1)
“Nyakati” na “siku” hapa si tarehe za kawaida katika kalenda. Ayubu anauliza kuhusu majira yaliyowekwa kwa ajili ya hukumu—siku ambazo Mungu huweka wazi na kunyoosha yaliyopotoka. Wale wanaomjua Mungu huzitamani siku hizo kama walinzi wanavyoingojea asubuhi.
Lakini asubuhi haifiki.
Swali hili liko katikati ya maombolezo ya kibiblia. Manabii nao hulia, “Hata lini?” (Habakuki 1:2; Zekaria 1:12). Watunga zaburi huuliza kwa nini waovu wanastawi huku maskini wakikandamizwa (Zaburi 10:1–11; 73:3–12; 94:3–7). Habakuki anauliza kwa nini Mungu anaiona dhuluma lakini anaonekana kunyamaza (Habakuki 1:2–4, 13). Ayubu anaungana na kwaya hiyo ya imani iliyojeruhiwa, akiuliza kwa nini waovu wanaendelea kuishi, kustawi, na kutawala huku wanaoteseka wakilia bila kupata msaada (Ayubu 21:7–15; 24:1–12).
Ni muhimu kubaini kuwa Ayubu hapingi uwepo wa siku za Mungu za utekelezaji wa haki, bali anahoji sababu za kufichika kwake. Hakanushi nafasi ya Mungu kama Mwamuzi Mkuu, bali anahoji kuchelewa kwa maamuzi yake. Suala hapa si ukosefu wa imani—ni mateso ya kusubiria haki iliyoahirishwa.
Suala hilo bado linatesa hata leo. Kwa nini viongozi mafisadi wamalize siku zao kwa starehe na anasa? Kwa nini wenye jeuri wakimbie hukumu ya uovu wao? Kwa nini masikini waendelee kusubiri haki miaka nenda miaka rudi? Kwa nini vyombo vya sheria vichelee kutoa haki na kusaliti matumaini? Kwa nini kilio cha wajane kishie hewani bila majibu? Na kwa nini watoto wawe wahanga wa mifumo iliyoharibiwa na watu wazima?
Ayubu anatufundisha kwamba maswali kama haya yana nafasi ndani ya lugha ya imani. Si ishara kwamba imani imekufa. Huenda yakawa ishara kwamba dhamiri bado iko hai.
Imani isiyouliza kamwe kwa nini haki inachelewa huenda imeacha kusikiliza vilio vya wanaodhulumiwa.
3.2 Mawe ya Mipaka na Mifugo Iliyoibwa: Nguvu Inapoiba Ardhi na Riziki (24:2–3)
Ayubu anaanza ushahidi wake kwa wizi wa ardhi:
“Watu huhamisha alama za mipaka; huchukua makundi ya mifugo na kuyachunga. Humfukuza punda wa yatima; humchukua ng’ombe wa mjane kuwa rehani.” (24:2–3)
Uhalifu huu ni wa wazi. Kuhamisha mawe ya mipaka hakukuwa kitendo kidogo cha udanganyifu wa mtu binafsi. Ilikuwa shambulio dhidi ya urithi, uhai wa familia, na utaratibu wa agano. Ardhi haikuwa mali tu; ilikuwa riziki, kumbukumbu, na mahali pa kuishi. Kuhamisha alama ya mpaka kulikuwa kufuta wakati ujao wa familia hatua kwa hatua.
Kisha waovu wananyakua mifugo. Katika ulimwengu wa kale, mifugo ilikuwa utajiri, chakula, kazi na uhai. Kuiba kundi la mifugo kulikuwa kama kuyang’oa mapafu ya kiuchumi ya nyumba.
Picha zinazofuata zinawaangazia walio dhaifu zaidi: yatima na mjane. Punda wa yatima anachukuliwa. Ng’ombe wa mjane anakamatwa kuwa rehani. Wanyama hawa si vitu vya anasa. Ni zana za kuishi. Bila wao, walio dhaifu hawawezi kufanya kazi, kusafiri, kulima, kubeba mizigo, wala kuendeleza maisha yao yaliyo hatarini.
Hii ndiyo sababu Torati na Manabii hukazia ulinzi kwa wajane, yatima, na maskini (Kutoka 22:21–24; Kumbukumbu la Torati 10:17–18; 24:17–22; Isaya 1:16–17; Zekaria 7:9–10). Moyo wa jamii yoyote haupimwi kwa jinsi inavyowalea wenye nguvu, bali kwa jinsi inavyowakinga wasio na mtetezi.
Zaidi ya hayo, orodha anayotoa Ayubu inajibu tuhuma za Elifazi kwa utulivu na umakini mkubwa. Uhalifu uleule aliosingiziwa na Elifazi, sasa Ayubu anaulaani kwa msimamo usiotikisika wa kimaadili (Ayubu 22:7–9; 24:3–12). Ayubu anawashuhudia wahanga na kuijua vyema sheria ya huruma—yeye si yule mnyonyaji aliyebuniwa katika mawazo ya Elifazi, bali mtu ambaye baadaye anathibitisha kwamba hakuwahi kuwanyima maskini, wajane, wala yatima msaada wao (Ayubu 29:12–17; 31:16–23).
Mwenye haki anayeteseka habakii kwenye maumivu yake; anakuwa jicho na sauti ya mateso ya wenzake.
3.3 Maskini Wanasukumwa Kando ya Barabara: Wanyonge Wanapolazimika Kujificha (24:4–8)
Ayubu anaendelea:
“Huwasukuma maskini waondoke njiani; maskini wote wa nchi hulazimika kujificha.” (24:4)
Huku si kuondolewa mahali tu. Ni kufutwa katika maisha ya jamii. Maskini wanasukumwa nje ya nafasi za umma. Wanalazimishwa kujificha. Barabara inamilikiwa na wenye nguvu. Walio dhaifu hulazimika kupita kwa tahadhari, kimya, kana kwamba hawaonekani.
Kisha Ayubu anawalinganisha na punda-mwitu wa jangwani:
“Kama punda-mwitu jangwani, maskini hutoka kwenda kufanya kazi yao, wakitafuta chakula; nyika huwapatia chakula watoto wao.” (24:5)
Picha inayochorwa hapa ni ya kusikitisha mno. Wanadamu walioumbwa kwa mfano wa Mungu wanaishi kama wanyama wanaowindwa, wakitafuta mabaki ya kuendesha maisha yao katika maeneo makavu. Jasho lao halileti utulivu wala furaha, bali ni mapambano ya kukata tamaa; hawavuji jasho ili kustawisha maisha, bali wanapambana usiku na mchana ili watoto wao wasife kwa njaa.
Maskini wanaokota masazo mashambani na katika mizabibu (Ayubu 24:6). Lakini hapa kuna uchungu mkubwa: tendo ambalo Torati ililiweka kuwa ngao ya huruma kwa maskini, wageni, yatima, na wajane, limegeuzwa kuwa uwanja wa unyonyaji (Mambo ya Walawi 19:9–10; 23:22; Kumbukumbu la Torati 24:19–21). Wanyonge hawa wanaokota makombo kwenye kingo za utajiri wa wengine, wakipigania kuishi katikati ya ulimwengu uliosahau utu wao (Ayubu 24:10–12; Amosi 8:4–6).
Kisha baridi ya usiku inaingia:
“Hulala usiku kucha wakiwa uchi, bila nguo, wala hawana kifuniko wakati wa baridi. Hunyeshewa na mvua za milimani, na kwa kukosa makao hujishikiza kwenye mwamba.” (24:7–8)
Taswira hii inagusa hadi undani wa mifupa. Maskini si takwimu. Ni ngozi iliyoganda, mavazi yaliyolowa, watoto wanaotetemeka, matumbo matupu, na migongo iliyotupwa kwenye jiwe. Ayubu anatufanya tuihisi mvua yenyewe ikitunyeshea.
Hii ndiyo sauti ya haki ya kinabii na kibiblia: inakataa kuyaacha mateso yawe wazo lisilo na uso. Maandiko yanatuvuta karibu kiasi cha kutufanya tusikie kilio na kuushuhudia mwili unaotetemeka kwa baridi na dhiki.
Dhuluma si hitilafu tu katika mfumo; ni baridi kali ya usiku inayopenya na kuuma ndani ya ngozi ya mwanadamu.

3.4 Watoto Wanachukuliwa na Wafanyakazi Wanaachwa na Njaa: Uchumi Unapowala Wanyonge (24:9–11)
Ayubu anaongeza ukali wa picha:
“Wapo wanaomnyakua mtoto yatima kutoka kifuani, na kuchukua rehani kutoka kwa maskini.” (24:9)
Taswira ya mtoto anayenyakuliwa kutoka kifuani mwa mama yake inachoma moyo na haivumiliki. Inafichua utumwa wa madeni, unyang'anyi wa watoto, na unyonyaji wa kinyama dhidi ya maskini. Hoja kuu hapa haina utata: walio na mamlaka wanaigeuza damu na nyama ya maskini kuwa dhamana ya madeni. Kiungo cha ndani kabisa cha upendo—kati ya mtoto na mama yake—kinasambaratishwa na uchu wa mali uliokosa utu.
Kisha Ayubu anaelezea wafanyakazi wanaofanya kazi wakiwa na njaa:
“Hutembea uchi, bila nguo; wakiwa na njaa hubeba miganda ya nafaka; katika safu za mizeituni za waovu hukamua mafuta; hukanyaga mashinikizo ya divai, lakini wao wenyewe wana kiu.” (24:10–11)
Hii ni mojawapo ya picha kali zaidi za unyonyaji katika Maandiko. Maskini hubeba nafaka lakini hubaki na njaa. Hukamua mafuta lakini hawapati faraja. Hukanyaga zabibu lakini wana kiu. Wamezungukwa na chakula na kinywaji, lakini wananyimwa matunda ya kazi ya mikono yao.
Huu si wizi wa mabavu pekee—ni unyonyaji uliorasimishwa kisheria na kimfumo. Ni mfumo unaomkamua mfanyakazi ili kuzalisha neema, huku ukimwacha mhusika akiangamia kwa njaa. Katika mazingira haya, mavuno yanakuwa ushahidi wa dhuluma, vyombo vya uzalishaji vinabadilika kuwa viwanja vya hukumu, na miganda inayobebwa na wajenzi wa uchumi hao waliokosa chakula inagoma na kushitaki mfumo mzima.
Baadaye Yakobo atasema kwa sauti inayofanana: mishahara iliyozuiliwa kwa wafanyakazi inapiga kelele, na vilio vya wavunaji vinafika masikioni mwa Bwana wa majeshi (Yak. 5:4). Ayubu 24 iko ndani ya sauti hiyo ya kinabii.
Hapa teolojia ya Ayubu inachana vipande vipande ucha Mungu wa maneno uliokosa utu wa matendo. Huwezi kujifanya unamwabudu Mungu huku ukinona kupitia mifumo inayowafanya wenye njaa wabebe chakula kisichoweza kuingia vinywani mwao! Hata wakati
wenye kiu wanapokamua zabibu kwenye shinikizo, ule uwingi wenyewe wa divai unageuka kuwa ushahidi unaopiga kelele dhidi ya dhuluma yao.
3.5 Maombolezo Yanayotoka Mjini: Mungu Anapoonekana Kutowashtaki Watenda Maovu (24:12)
Sasa Ayubu anahama kutoka mashambani kwenda mjini:
“Kutoka mjini wanaokufa huugua, na nafsi za waliojeruhiwa hulilia msaada; lakini Mungu haonekani kumhesabia mtu yeyote kosa.” (24:12)
Aya hii ndiyo iliyobeba maumivu ya sura nzima. Mji unaugua. Waliojeruhiwa wanalia. Wanaokufa hawako kimya. Sauti zao zinapanda kutoka mitaani, vichochoroni, majumbani na malangoni.
Lakini Mungu anaonekana kutowawajibisha watenda maovu.
Huu si ufafanuzi wa teolojia uliokamilika na wenye mipaka safi. Ni maombolezo. Ayubu anaeleza namna hali halisi inavyohisiwa wakati dhuluma inaendelea bila kuzuiwa. Vilio vinasikika duniani, lakini mbingu inaonekana kutotoa hati ya mashtaka.
Hapa Ayubu anakaribia kumshutumu Mungu—si kwamba Mungu anatenda uovu moja kwa moja, bali kwamba hachukui hatua dhidi ya uovu kwa haraka inayotarajiwa. Hilo ni ombi hatari, lakini Maandiko yamelihifadhi kwa sababu majeraha ya ulimwengu yanahitaji lugha ya kweli.
Biblia haitufundishi kuuita uovu kuwa wema. Haiwaombi waliojeruhiwa kuusifu ukimya wa mahakama. Inaruhusu kilio hiki: “Waliojeruhiwa wanaita msaada, lakini Mungu anaonekana kutowashtaki waovu.”
Kwa wasomaji Wakristo, aya hii inapaswa kuwekwa karibu na msalaba. Huko pia, Yule asiye na hatia aliuwawa nje ya mji, akiwa amejeruhiwa na kuanikwa wazi, huku watu wenye mamlaka wakionekana kutoshtakiwa na kushinda. Lakini ufufuo unafunua kwamba kuchelewa kwa Mungu hakukuwa kushindwa kwa Mungu. Hata hivyo, Ijumaa Kuu inatufundisha tusiseme kwa wepesi juu ya ukimya uliopo kati ya kilio na jibu.
Kilio cha aliyejeruhiwa hakipotei kamwe, hata hukumu inapoonekana kuchelewa.

3.6 Waasi Dhidi ya Nuru: Mauaji, Uzinzi na Wizi wa Usiku (24:13–17)
Sasa Ayubu anaelezea kundi jingine la watenda maovu:
“Wapo wanaoiasi nuru, wasiozijua njia zake wala kukaa katika mapito yake.” (24:13)
Katika Maandiko, nuru mara nyingi humaanisha kweli, utaratibu, hekima, na ufunuo wa Mungu unaoyaweka mambo wazi. Watu hawa wanaasi nuru. Wanachagua giza si kwa sababu hawawezi kuona, bali kwa sababu hawataki kuonekana.
Ayubu anataja uhalifu wa aina tatu unaotendeka usiku:
Muuaji huamka kabla ya mapambazuko ili kuwaua maskini na wahitaji (24:14).
Mzinzi husubiri jioni, akisema, “Hakuna jicho litakaloniona” (24:15).
Wezi huvunja nyumba gizani, na wakati wa mchana hujifungia ndani (24:16).
Kwao, giza nene ndilo asubuhi (24:17).
Picha hii inaonyesha uovu kama uasi dhidi ya uumbaji. Katika Mwanzo, Mungu anaiita nuru kuwa njema. Hapa wenye dhambi wanafanya giza kuwa nyumbani kwao. Wanavuruga utaratibu wa uumbaji. Asubuhi inawatisha kwa sababu inawafunua. Giza linawafariji kwa sababu linawasitiri.
Kauli ya mzinzi inafunua mengi: “Hakuna jicho litakaloniona.” Hii ndiyo teolojia ya vitendo ya dhambi ya siri. Si lazima imkane Mungu kwa maneno. Inaishi kana kwamba kujificha ni kusalimika. Lakini Maandiko yanaonya tena na tena kwamba kinachofichika machoni pa wanadamu kinaendelea kuonekana mbele za Mungu.
Hata hivyo, malalamiko ya Ayubu yanabakia hewani: kama Mungu anaona, kwa nini hachukui hatua sasa?
Swali hili linaendelea kusalia bila majibu mepesi. Hata hivyo, kwa kuweka wazi uwepo wa giza hili, Ayubu anatekeleza tendo la kimkakati la upinzani wa kimaadili. Uovu hutegemea uficho na usiri ili kuendelea; Ayubu anaufichua kwa kuupa umbo la kimatamshi. Giza hushikilia nguvu zake wakati hakuna anayehoji; Ayubu anaiasi hali hiyo kwa kulitangaza wazi.
Kuukabili uovu na kuutaja kwa jina lake halisi tayari ni ushindi wa nuru mbele ya giza.
3.7 “Ni Mwepesi Juu ya Maji”: Mgeuko Mgumu Kuhusu Hatima ya Waovu (24:18–24)
Sehemu ya mwisho ya sura inabadilisha sauti. Ghafla shairi linazungumzia waovu kuwa wepesi juu ya maji, sehemu yao kulaaniwa, ukame na joto kuyameza maji ya theluji, Kuzimu kuwameza watenda dhambi, tumbo la uzazi kuwasahau, minyoo kuwala, na kumbukumbu yao kuvunjwa kama mti.
Mistari hii inasikika karibu zaidi na teolojia ya marafiki: waovu wanahukumiwa, wanafutwa na kushushwa chini.
Hilo linaleta mvutano. Je, sasa Ayubu anakubaliana na marafiki zake? Je, ananukuu maneno yao? Je, anazungumza kwa kejeli? Je, anakiri kwamba wakati mwingine hukumu hufika? Au aya hizi zimehamishwa kutoka hotuba nyingine, labda hotuba ya tatu ya Sofari ambayo haipo?
Usomaji wenye hekima haupaswi kuufanya ugumu huu kuwa mwepesi kuliko ulivyo. Ayubu 24 yenyewe imekuwa ikifunua ulimwengu ambao haki haiji mara moja. Aya 18–24, zikisomwa kama maneno ya Ayubu, huenda zinaonyesha akishikilia uhalisi wa pande mbili: mara nyingi waovu hudhulumu bila kuadhibiwa, lakini mwisho wao bado uko chini ya hukumu ya Mungu. Ikiwa aya hizi ni sauti ya marafiki au sehemu iliyohamishwa, mahali zilipo bado panakitumikia kitabu kwa kutukumbusha madai yanayoshindana ndani ya mjadala.
Kwa vyovyote vile, mvutano huu una matunda ya kitheolojia. Maandiko yanafundisha kwamba waovu hawatashinda milele. Pia yanafundisha kwamba, kwa sasa, mara nyingi waovu hushinda. Imani lazima ijifunze kusema kweli zote mbili bila kutumia moja kunyamazisha nyingine.
Waovu wanaweza kusahauliwa na tumbo la uzazi, kuliwa na minyoo, na kuvunjwa kama mti. Hata hivyo, maskini wanaweza bado kuwa na njaa leo. Kuanguka kwa uovu siku ya mwisho hakufuti kilio cha sasa cha haki.
Hukumu ya baadaye si ruhusa ya kutojali leo.
3.8 “Ni Nani Atakayethibitisha Nimesema Uongo?”: Changamoto ya Ayubu kwa Wafariji (24:25)
Ayubu anafunga kwa changamoto:
“Kama mambo si hivyo, ni nani atakayethibitisha kwamba mimi ni mwongo na kuonyesha kuwa maneno yangu hayana uzito?” (24:25)
Huku si kujivuna. Ni kutoa ushahidi. Ayubu anasema: Utazame ulimwengu. Waulize maskini. Tembea mashambani. Sikiliza mjini. Tazama usiku. Ukiona nina makosa, niambie.
Marafiki wamejenga teolojia yao wakianzia kwenye kanuni na kushuka kwenda kwenye maisha. Ayubu anajenga malalamiko yake akianzia kwenye hali halisi na kupanda kwenda kwenye teolojia. Hakatai wamba Mungu ni mwenye haki. Anachokataa ni teolojia inayojifanya kipofu kutambua kuwa wakati mwingine haki huchelewa.
Changamoto hii ya mwisho pia inaonyesha ujasiri wa Ayubu. Licha ya kukabiliwa na mashtaka ya uongo, haishii tu kwenye kujitetea nafsi yake, bali anachukua nafasi ya kuwa shahidi wa wote wanaokabiliwa na dhuluma. Maumivu aliyopitia hayakumfanya asahau wajibu wake wa kimaadili—yaliifanya akili yake iwe macho zaidi kuona uonevu na kuupinga.
Rundo la majivu ya Ayubu limegeuka kuwa kizimba cha shahidi.
4.0 Tafakari ya Kitheolojia: Mungu Ambaye Haki Yake Ni Halisi, Ingawa Haiji Mara Moja Kila Wakati
Ayubu 24 inatufundisha kukataa makosa mawili.
Kosa la kwanza ni kosa la marafiki: kuamini kwamba haki huja mara moja kila wakati, huonekana wazi, na ni rahisi kuitafsiri. Mtazamo huu huzaa ukatili. Hutufanya tuwalaumu wanaoteseka, kuitetea mifumo ya dhuluma, na kuzitafsiri hali za maisha kana kwamba ni hukumu za Mungu.
Kosa la pili ni kukata tamaa: kuamini kwamba kwa sababu haki inachelewa, basi haki si halisi. Ayubu hafiki huko pia. Anamwuliza Mungu kwa ukali, lakini anaendelea kusema kama mtu anayeamini kwamba hukumu ya Mungu ina maana. Swali lake—“Kwa nini Mwenyezi haweki nyakati?”—lina maana tu kama Mwenyezi ndiye anayepaswa kuweka nyakati hizo.
Mvutano huu unapatikana katika Biblia nzima. Ibrahimu anauliza, “Je, Mwamuzi wa dunia yote hatatenda haki?” (Mwanzo 18:25). Musa anaijenga sheria ya Israeli kuzunguka ulinzi wa maskini, mjane, yatima na mgeni (Kutoka 22:21–24; Kumbukumbu la Torati 10:17–19; 24:17–22). Manabii wananguruma dhidi ya wale wanaouza wenye haki kwa fedha na wahitaji kwa jozi ya viatu (Amosi 2:6–7; 8:4–6). Watunga zaburi wanalia juu ya ustawi wa waovu (Zaburi 73:2–12; 94:3–7). Yesu anawatangazia maskini habari njema na kutamka ole juu ya wale wanaomeza nyumba za wajane (Luka 4:18–19; 6:20–24; Marko 12:38–40).
Ayubu 24 imo ndani ya mto huo.
Lakini sura hii inaongeza jambo la pekee: anayeteseka anakuwa mwanateolojia wa haki ya jamii. Ayubu si mgonjwa anayejililia mwenyewe tu; ni shahidi wa maadili. Akiwa kwenye majivu, anaona yale ambayo wenye starehe huyapuuza—wafanyakazi wenye njaa kando ya mavuno, maskini waliolowa chini ya miamba, waliojeruhiwa wakiugua mjini, na waovu wanaotumia giza kama pazia la uhalifu wao (Ayubu 24:5–12, 14–17).
Hili ni muhimu kitheolojia kwa sababu haki ya Mungu haihusu tu hatima ya mtu mmoja mmoja. Inahusu mpangilio wa ulimwengu. Marafiki wanaipunguza haki kuwa hesabu ya mtu binafsi: Ayubu anateseka, kwa hiyo Ayubu ametenda dhambi. Ayubu anaipanua haki mpaka ihusishe ardhi, kazi, miili, watoto, mahakama, mitaa na uhalifu wa usiku.
Maono haya mapana yana mizizi ya kina katika Biblia. Dhambi si doa la moyoni pekee; inaweza pia kujenga mifumo ya jeuri na unyonyaji. Haki si kutokuwa na hatia binafsi tu; ni uaminifu unaoonekana katika namna tunavyowatendea wengine na kuunda maisha ya pamoja.
Kwa wasomaji Wakristo, Ayubu 24 inatuelekeza kwa Yesu kwa angalau njia tatu.
Kwanza, Yesu anasimama upande wa maskini, waliotengwa, na walioachwa bila mtetezi. Anawatangazia maskini habari njema, anawagusa waliotengwa, anawalisha wenye njaa, anawakaribisha watoto, na kuzikemea mifumo ya kidini inayowabebesha wanyonge mizigo mizito (Luka 4:18; Marko 1:40–42; 6:34–44; 10:13–16; Mathayo 23:4).
Pili, Yesu mwenyewe anaingia ndani ya dhuluma anayoieleza Ayubu. Anashtakiwa kwa uongo, anavuliwa nguo, anadhihakiwa, anajeruhiwa, na kuuawa nje ya mji. Usiku wa usaliti, jeuri ya mamlaka, na ukimya wa haki vinakusanyika juu yake (Marko 14:55–65; 15:15–20; Yohana 19:23–24; Waebrania 13:12).
Tatu, ufufuo wa Yesu ni alfajiri ya siku ya haki ya Mungu. Bado haujakomesha kila dhuluma, lakini unathibitisha kwamba Mungu ameweka siku ya kuuhukumu ulimwengu kwa haki. Ufufuo unasema kwamba kilio cha wanaoteseka kimesikika, giza limevamiwa, na Mwamuzi wa mwisho tayari ametangazwa (Matendo 17:31; Warumi 8:22–23; Ufunuo 21:4).
Kwa hiyo, Ayubu 24 inatufundisha tumaini lisilofumba macho mbele ya ukweli. Hatuifichi kuchelewa kwa haki, wala kujifanya kwamba maskini wako salama huku wakipondwa. Hatuibariki mifumo inayowanyonya wafanyakazi na kuiita ya haki. Lakini pia hatuukabidhi ulimwengu kwa giza.
Haki ya Mungu inaweza kuonekana kuchelewa, lakini haijakufa; siku yake inakuja.
5.0 Matumizi Katika Maisha: Kujifunza Kuona Yale Aliyoona Ayubu
5.1 Uliza Maswali Bora Kuhusu Haki
Ayubu haulizi tu, “Kwa nini ninaumia?” Anauliza, “Kwa nini wanaodhulumiwa wanasubiri?” Imani iliyokomaa hujifunza kuuliza yote mawili. Mateso yetu binafsi hayapaswi kutufanya tusijali mateso ya jamii. Wakati mwingine majeraha yetu wenyewe yanaweza kutufundisha kuyaona majeraha tuliyokuwa tukiyapuuza.
5.2 Usigeuze Umaskini Kuwa Jambo la Kiroho Tu
Ayubu anazungumzia njaa, mavazi, makao, kazi, ardhi, deni na wizi. Haya ni mambo yanayogusa mwili na maisha ya kila siku. Imani ya kibiblia haiyaweki pembeni. Mwenye njaa anahitaji maombi, lakini pia anahitaji mkate. Aliyenyeshewa anahitaji huruma, lakini pia anahitaji kufunikwa. Mfanyakazi anahitaji kuombewa baraka, lakini pia anahitaji ujira wa haki.
5.3 Walinde Wanyonge Dhidi ya Mifumo Inayowanyang’anya Zana za Kuishi
Punda wa yatima na ng’ombe wa mjane vinawakilisha nyenzo za msingi za kujipatia riziki. Katika ulimwengu wa leo, tunaweza kufikiria mshahara, zana za kazi, upatikanaji wa ardhi, makazi, nyaraka, elimu, huduma za afya, na ulinzi wa haki mbele ya sheria. Haki hulinda yale ambayo wanyonge wanahitaji ili waendelee kuishi.
5.4 Lilete Giza Kwenye Nuru
Ayubu anataja uhalifu unaopenda kujificha. Makanisa na jamii hazipaswi kulilinda giza kwa ajili ya sifa, urafiki, fedha au mamlaka. Unyanyasaji, unyonyaji, wizi na usaliti lazima viwekwe mbele ya ukweli. Ukimya unaweza kuwa makao ya uovu.
5.5 Shikilia Maombolezo na Tumaini Pamoja
Ayubu 24 inatufundisha sanaa ya kuombolezea haki inayochelewa bila kupoteza imani katika hukumu ya mwisho. Inatupa idhini ya kulia, ‘Hata lini, Bwana?’ huku tukiendelea kushikilia ahadi ya uingiliaji kati wake. Inatupa ujasiri wa kuitaja dhuluma ya leo kwa jina lake, huku macho yetu yakiwa yamekazwa kwenye Siku ya Bwana inayokuja.
Tumaini la Kikristo si kuukimbia ukweli; ni msimamo thabiti wa imani kwamba pambazuko la Mungu litashinda giza nene la usiku wowote.
6.0 Maswali ya Kutafakari
Ayubu 24 inatufundisha nini kuhusu uhusiano kati ya mateso ya mtu mmoja na mifumo ya dhuluma inayoumiza jamii nzima?
Kwa nini swali la Ayubu kuhusu “nyakati” na “siku” za Mungu ni muhimu katika kuelewa kuchelewa kwa haki?
Ni picha ipi katika Ayubu 24 inayokufunulia kwa nguvu zaidi uchungu na ukatili wa dhuluma? Kwa nini?
Kujali kwa Ayubu maskini, wajane, na yatima kunajibuje mashtaka ya Elifazi katika Ayubu 22:6–9?
Ni wapi katika jamii ya leo tunawaona watu wakibeba “miganda” ya utajiri wa wengine huku wao wenyewe wakibaki na njaa?
Ni aina gani za giza—ukimya, hofu, siri, mamlaka au rushwa—zinazoruhusu uovu kujificha katika familia, makanisa, jamii na mataifa?
Kifo na ufufuo wa Yesu vinaimarishaje tumaini letu kwamba Mungu ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki?
7.0 Sala ya Mwitikio
Bwana Mungu,
Unasikia maombolezo yanayotoka mjini.
Unawaona maskini wakisukumwa waondoke njiani.
Unamjua mtoto anayenyakuliwa kifuani, mjane anayenyang’anywa ng’ombe wake, mfanyakazi mwenye njaa anayebeba nafaka, na mwenye kiu anayekanyaga zabibu katika shinikizo la divai.
Tufundishe kuyaona yale aliyoyaona Ayubu.
Utusamehe kwa nyakati tulizotetea majibu mepesi huku wanyonge wakiteseka. Utusamehe kwa maneno ya kiroho ambayo hayakugeuka kuwa mkate, huruma ambayo haikugeuka kuwa makao, na maombi ambayo hayakugeuka kuwa matendo ya haki.
Yalete mambo yaliyofichika katika nuru yako. Uufunue uhalifu unaoupenda usiku. Watie nguvu waliochoka, wavike walio uchi, walishe wenye njaa, walinde wajane na yatima, na uwafanye watu wako kuwa makao katika ulimwengu wenye dhoruba.
Na haki inapochelewa, ulilinde tumaini letu lisizimike. Utupe ujasiri wa kuomboleza bila kukata tamaa, kusubiri bila kujidanganya, na kufanya kazi bila mioyo yetu kupoa.
Katika jina la Yesu Kristo, aliyejeruhiwa nje ya mji na kufufuliwa kama mapambazuko ya haki yako inayokuja,
Amina.
8.0 Dirisha la Sura Inayofuata: Bildadi Anapompunguza Mwanadamu Mbele za Mungu
Ayubu 24 inamalizika kwa changamoto ya Ayubu: ni nani anayeweza kuthibitisha kwamba amekosea? Ameeleza ulimwengu ambamo maskini wanapondwa, waovu wanajificha gizani, na haki inaonekana kuchelewa.
Katika Ayubu 25, Bildadi anatoa hotuba yake ya mwisho. Ni fupi—fupi kwa namna inayoshangaza. Maneno ya marafiki yanaanza kuwaisha. Bildadi haujibu ushahidi wa Ayubu. Anarudi kwenye mada aliyoizoea: Mungu ni mwenye enzi kuu, mwanadamu si safi, na hakuna aliyezaliwa na mwanamke anayeweza kuwa mwenye haki mbele zake.
Sura inayofuata itatuleta kwenye wakati mdogo lakini muhimu katika mjadala: marafiki wanaposhindwa tena kueleza mateso ya Ayubu, wanakuza uchafu wa mwanadamu na kumwacha mwenye mateso bila jibu.
Ayubu 25 itauliza kinachotokea wakati heshima kwa Mungu inapogeuka kuwa dharau kwa mwanadamu.
9.0 Bibliografia
Alter, Robert. The Wisdom Books: Job, Proverbs, and Ecclesiastes: A Translation with Commentary. New York: W. W. Norton, 2010.
BibleProject. The Book of Job: Guide with Key Information and Resources. Portland: BibleProject, 2026.
Clines, David J. A. Job 21–37. Word Biblical Commentary 18A. Nashville: Thomas Nelson, 2006.
Hartley, John E. The Book of Job. New International Commentary on the Old Testament. Grand Rapids: Eerdmans, 1988.
Newsom, Carol A. The Book of Job: A Contest of Moral Imaginations. Oxford: Oxford University Press, 2003.
Walton, John H., and Tremper Longman III. How to Read Job. Downers Grove: IVP Academic, 2015.




Comments